Na: OWM (KAM) - Dodoma
Serikali imeendelea kuhakikisha miradi mikubwa inayotekelezwa ama inayoanzishwa inatoa fursa za Ajira kwa Watanzania zaidi.
Aidha, utekelezaji wa suala hilo linatekelezwa kupitia utekelezaji wa Sera na Sheria ambapo miongoni mwa Sera na Sheria hizo ni pamoja na Sera ya Taifa ya Ajira ya mwaka 2008, Sera ya Taifa ya Nishati ya mwaka 2015, Sheria ya Mafuta, Sura 392 pamoja na Sheria ya Madini Sura 123.
Hayo yamebainishwa Aprili 9, 2026 Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Rahma Kisuo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Jasmine Chesco, lililouliza Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha vijana wanapata ajira katika miradi mikubwa kama SGR na viwanja vya ndege.
Akijibu swali hilo, Mhe. Rahma amesema Kupitia miradi mikubwa inayotekelezwa nchini, vijana wananufaika na fursa za ajira ambapo zaidi ya ajira 35,000 zimetolewa katika ujenzi wa Reli ya SGR, zaidi ya ajira 10,000 katika mradi wa ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), na zaidi ya ajira 2,497 zimetolewa katika ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato Dodoma sambamba na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.
Vilevile, amesema zaidi ya ajira 1,500 zimetolewa katika ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi, na zaidi ya ajira 3,000 katika upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine, Mhe. Rahma amesema Serikali inahakikisha vijana wanapata ujuzi unaohitajika katika miradi hiyo kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi inayowawezesha vijana kupata ajira na kushiriki kwa ufanisi katika kazi za viwandani na miradi mikubwa ya kimkakati.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Rahma Kisuo


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...