Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imetoa utaratibu rasmi wa uombaji wa vibali vya kusimika mabango kando ya barabara, ikiwa ni hatua ya kukabiliana na matapeli wanaojifanya watumishi wa taasisi hiyo na kuwahadaa wafanyabiashara.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wananchi wanaotaka kuweka mabango wanapaswa kuwasilisha maombi yao kwa njia ya barua rasmi kwa wakala, wakieleza kwa kina ujumbe wa tangazo, ukubwa wa bango (kwa mita za mraba), pamoja na namba ya simu ya mawasiliano.
Hatua inayofuata itahusisha ukaguzi wa eneo lililopendekezwa kufungwa bango, ambapo maafisa wa TANROADS watathibitisha kama eneo hilo linakidhi vigezo vinavyotakiwa, Endapo mwombaji atakidhi vigezo, atapewa barua ya malipo yenye namba ya kumbukumbu (control number) kwa ajili ya kukamilisha malipo husika.
Baada ya kufanya malipo, mwombaji atapatiwa kibali rasmi cha kusimika bango, ambacho kitakuwa halali kwa kipindi cha mwaka mmoja, TANROADS imefafanua kuwa baada ya muda huo kuisha, mmiliki wa bango atalazimika kulipia upya ili kuhuisha kibali chake na kuendelea kutumia eneo hilo.
Wakala huo umewataka wananchi kuwa makini na watu wanaojitambulisha kama watumishi wake bila uthibitisho rasmi, na kusisitiza kuwa taratibu zote za maombi na malipo zinapaswa kufanywa kupitia njia rasmi zilizoainishwa.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...