Na Janeth Raphael- MichuziTv -Dodoma
Tanzania imepata heshima kubwa ya kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Pili wa Mwaka wa Jumuiya za Wataalamu wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Utawala Bora barani Afrika, tukio litakalowakutanisha wataalamu kutoka mataifa mbalimbali kwa lengo la kubadilishana uzoefu, kujengeana uwezo na kuimarisha mifumo ya utumishi wa umma katika bara la Afrika.
Mkutano huo mkubwa umepangwa kufanyika kuanzia tarehe 5 hadi 8 Mei, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), ambapo Tanzania itawakilishwa na taasisi zote zilizo chini ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 29, 2026 jijini Dodoma, Mwenyekiti wa African Association for Public Administration and Management (AAPAM) Tanzania Chapter, Leila Mavika, amesema maandalizi ya mkutano huo yamekamilika kwa kiwango kikubwa na unatarajiwa kuwa na matokeo chanya kwa maendeleo ya utawala bora barani Afrika.
Mavika alieleza kuwa mkutano huo umeandaliwa na AAPAM, taasisi inayojumuisha nchi zote wanachama barani Afrika kupitia matawi yake ya kitaifa, ambapo Tanzania ina AAPAM Tanzania Chapter inayoratibiwa chini ya Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kama mlezi wa taasisi hiyo nchini.
Ameongeza kuwa mkutano huo wa pili wa mwaka utakuwa jukwaa muhimu la kitaaluma litakalowakutanisha wataalamu wa utawala wa umma, usimamizi wa rasilimaliwatu na utawala bora kutoka nchi mbalimbali za Afrika, kwa lengo la kujadili changamoto, fursa na mbinu bora za kuboresha utendaji wa sekta ya umma.
Aidha, Mavika amebainisha kuwa mkutano huo utashirikisha pia Jumuiya ya Wataalamu wa Utawala wa Umma na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Tanzania (TAPAHR) pamoja na Mtandao wa Mameneja wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Tanzania (TPS-HRMnet), katika kuimarisha ushirikiano wa kitaaluma na kikanda.
Katika hatua nyingine, ametoa wito kwa waajiri wote katika Wizara, Tawala za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wakala za Serikali, Mashirika ya Umma, Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati kuhakikisha wanawapatia wataalamu wao wa utumishi wa umma nafasi ya kushiriki kikamilifu katika mkutano huo.
Amesema ushiriki huo utawasaidia kuongeza ujuzi, kubadilishana uzoefu na kuimarisha utendaji kazi katika maeneo yao ya kazi, hatua ambayo itachangia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma kwa wananchi.
Mkutano huo unatarajiwa kuwa moja ya matukio makubwa ya kikanda katika mwaka 2026, ukiweka Tanzania katika ramani ya uongozi wa mijadala ya utawala bora na maendeleo ya rasilimaliwatu barani Afrika.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...