Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kupitia Kitengo cha Uhusiano ikishirikiana na Kitengo cha Malalamiko ya Watumiaji wa Usafiri wa Anga Nchini (CCU), imeendelea na kampeni yake ya uhamasishaji kwa umma yenye kauli mbiu “Tiketi Yako, Haki Yako”, kwa lengo la kutoa elimu kwa watumiaji wa huduma za usafiri wa anga kuhusu haki na wajibu wao pindi wanapotumia huduma hizo.
Kampeni hiyo imefanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume(AAKIA), Zanzibar, Aprili 1, 2026, ambapo maafisa wa TCAA waliwafikia abiria na wadau mbalimbali kwa kutoa elimu ya ana kwa ana kupitia vipeperushi, mazungumzo ya moja kwa moja pamoja na kujibu maswali yanayohusu changamoto zinazowakabili wasafiri wa anga.
Kupitia kampeni hiyo, TCAA imewaelimisha watumiaji wa usafiri wa anga kuhusu haki zao, ikiwemo haki ya kupata taarifa sahihi kuhusu safari zao, haki ya fidia endapo safari itachelewa au kufutwa bila sababu za msingi, pamoja na wajibu wa kufuata taratibu na kanuni za usafiri wa anga. Aidha, elimu ilitolewa kuhusu njia sahihi za kuwasilisha malalamiko yao kwa TCAA ili yafanyiwe kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.
Lengo la kampeni hii ni kuhakikisha kuwa watumiaji wa huduma za usafiri wa anga wanafahamu haki zao na wanajua mahali sahihi pa kuwasilisha malalamiko yao wanapokumbana na changamoto, badala ya kukata tamaa au kutumia njia zisizo rasmi.
Kampeni hii ni endelevu na itaendelea kutekelezwa katika viwanja mbalimbali vya ndege nchini kama sehemu ya mkakati wa TCAA wa kulinda maslahi ya watumiaji wa usafiri wa anga na kuboresha utoaji wa huduma katika sekta ya anga.
Meneja Uhusiano TCAA, Ally Changwila akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kampeni yao ya uhamasishaji kwa umma yenye kauli mbiu “Tiketi Yako, Haki Yako”, kwa lengo la kutoa elimu kwa watumiaji wa huduma za usafiri wa anga kuhusu haki na wajibu wao pindi wanapotumia huduma hizo.
Watumishi wa TCAA wakiendelea kutoa elimu kwa abiria mbalimbali katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume(AAKIA), Zanzibar




.jpeg)
.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...