Wanamichezo wanaoshiriki mashindano ya UMISSETA jijini Dodoma wameaswa kuendelea kujituma katika mazoezi ili kuhakikisha Wilaya ya Dodoma inakuwa na timu imara ambayo itaweza kutetea makombe 13 yaliyopatikana katika msimu uliopita
Akizungumza wakati wa hafla ya kufunga mashindano hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Dodoma Afisa Michezo Jiji, Peter Iiti alisema kuwa lengo kuu la mashindano hayo ni kupata wachezaji bora watakaounda timu imara ya Wilaya yenye uwezo wa kushindana na kuleta matokeo chanya katika ngazi ya mkoa.
“Tumeshuhudia ushindani mkubwa wenye kuonesha vipaji vya hali ya juu kutoka kwa wanafunzi wetu. Hii ni ishara kuwa tuna hazina kubwa ya vipaji ambavyo vinahitaji kuendelezwa kwa umakini mkubwa.
“ikumbukwe kuwa kambi ya Wilaya itaanza Juni 4, 2026 kwaajili ya mashindano ya kujiandaa na UMISSETA ngazi ya Mkoa ikiwa kambi yake itaanza Juni 8, 2026 kwaajili ya kuunda timu ya Mkoa itakayoshirikia mashindano ngazi ya Taifa,” alisema Ititi.
Aliongeza kuwa michezo ni nyenzo muhimu katika kukuza nidhamu, afya njema pamoja na kuimarisha mshikamano miongoni mwa wanafunzi, hivyo akawataka walimu na wadau wa elimu kuendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha wanafunzi kushiriki kikamilifu katika shughuli za michezo.
“Ni wajibu wetu kuhakikisha tunakuza michezo mashuleni ili vijana wetu waweze kupata fursa ya kuonesha vipaji vyao na hatimaye kufikia ndoto zao. Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuboresha miundombinu ya michezo,” alisisitiza Ititi
Kwa upande wake, mmoja wa walimu walioshiriki katika maandalizi ya mashindano hayo Mwl, Kaizerege Tehingisa amabye ni Mwenyekiti wa TAHOSSA Halamshauri ya Jiji la Dodoma, alisema kuwa mashindano hayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kubaini vipaji vipya pamoja na kuimarisha ushindani wa michezo katika shule za jiji hilo.
“Tumepata wachezaji wazuri sana ambao tuna imani wataiwakilisha vyema wilaya katika ngazi ya mkoa. Kikubwa tunachosisitiza ni kuendelea kufanya mazoezi na kuwa na nidhamu ya hali ya juu,” alisema mwalimu huyo.
Baadhi ya wanafunzi walioshiriki mashindano hayo walieleza furaha yao kwa kushiriki na kupata uzoefu mpya, wakisema kuwa ni fursa muhimu kwao kujifunza na kujiendeleza kimichezo.
Akizungumza kwaniaba yao, Christina Mbuko alisema “Nimejifunza mambo mengi kupitia mashindano haya, ikiwemo kushirikiana na wenzangu na kujituma zaidi uwanjani. Nitajitahidi kufanya vizuri zaidi katika hatua inayofuata,” alisema Mbuko.
Mashindano hayo yalihusisha shule mbalimbali za Sekondari ndani ya Jiji la Dodoma, ambapo vipaji vilichaguliwa kwa kuzingatia uwezo wa mchezaji, nidhamu pamoja na ushirikiano wa timu.
Timu iliyoundwa sasa inatarajiwa kuanza maandalizi rasmi kwa ajili ya kushiriki mashindano ya UMISSETA ngazi ya Mkoa.
Serikali kupitia Idara ya Michezo imeendelea kusisitiza umuhimu wa michezo mashuleni kama sehemu ya kukuza vipaji na kuandaa kizazi chenye afya bora na uwezo wa kushindana kitaifa na kimataifa.
.jpeg)



.jpeg)

.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...