Na Mwandishi Wetu

Katibu Mkuu wa TRAMEPRO, Boniventura Mwalongo, ametoa wito maalumu kwa vijana nchini, Afrika Mashariki na duniani kote kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta ya tiba asili na uhifadhi wa mazingira, akizitaja kuwa ni nguzo muhimu za ajira, uchumi na maendeleo endelevu.

Akizungumza kupitia ujumbe wake maalumu kwa vijana, Mwalongo amesema dunia ya sasa imejaa fursa nyingi, lakini zinahitaji vijana wenye maarifa, ubunifu na uthubutu ili kuzitumia kikamilifu.

Amesema takwimu zinaonyesha kuwa takribani asilimia 80 ya watu duniani hutegemea tiba asili kwa huduma za afya za msingi, huku zaidi ya asilimia 70 ya Waafrika wakitumia dawa asilia mara kwa mara. Aidha, sekta ya dawa asilia duniani inakadiriwa kuwa na thamani inayozidi dola za Marekani bilioni 100, hali inayoashiria ukubwa wa soko hilo.

“Mahitaji ya tiba asili ni makubwa kila siku, hivyo vijana wana nafasi ya kushiriki katika uzalishaji, usindikaji, ubunifu na usambazaji wa bidhaa hizi,” amesema.

Amebainisha kuwa fursa zilizopo ni pamoja na uzalishaji wa dawa asilia zilizo salama, ufungashaji wa kisasa, utafiti na uthibitishaji wa bidhaa, ufunguzi wa kliniki za tiba asili, pamoja na biashara ya ndani na kimataifa.

Katika sekta ya mazingira, Mwalongo amesema uchumi wa kijani unatarajiwa kuunda zaidi ya ajira milioni 24 duniani ifikapo mwaka 2030. Ameeleza kuwa Tanzania ina utajiri mkubwa wa mimea tiba na maliasili ambazo bado hazijachunguzwa kikamilifu, hivyo kutoa nafasi kwa vijana kuwekeza katika kilimo cha mimea tiba, uzalishaji wa bidhaa za asili, uhifadhi wa misitu na utalii wa mazingira.

Amesisitiza umuhimu wa kuongeza thamani ya bidhaa badala ya kuuza malighafi ghafi, akieleza kuwa hatua hiyo inaweza kuongeza kipato mara tatu hadi kumi, kufungua masoko ya kimataifa na kuongeza ajira kwa wengine.

Hata hivyo, amewataka vijana kuzingatia maadili na usalama katika taaluma hiyo kwa kufuata viwango na sheria, na kupinga matumizi ya tiba zisizo salama ili kulinda afya za jamii na taswira ya sekta hiyo.

Katika wito wake, Mwalongo amesisitiza kuwa huu si wakati wa kusubiri ajira bali ni wakati wa vijana kuziunda wenyewe kwa kutumia fursa zilizopo.

“Anza kidogo, lakini anza leo. Maendeleo ya kweli huanza na hatua ndogo ya uthubutu,” amesisitiza.

Aidha, ametoa wito maalumu kwa Wabunge Vijana duniani kutumia nafasi zao kusukuma ajenda ya tiba asili katika sera na sheria, ili kuitambua kama sekta rasmi yenye mchango mkubwa katika uchumi, elimu na utafiti wa kisayansi.

Amehitimisha kwa kusisitiza kuwa tiba asili na mazingira ni fursa za dhahabu kwa vijana, ambazo zikitumiwa kwa weledi zinaweza kujenga uchumi imara, kulinda afya za jamii na kuhifadhi urithi wa kizazi kijacho.

Kauli mbiu yake ikisema: “Tiba Asili ni Ajira, Mazingira ni Uhai—Vijana Chukueni Hatua Sasa!”

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...