Timu ya Vodacom Tanzania ikiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kukamilisha mabadiliko ya huduma ya M-Pesa kwenda mfumo mpya wa kisasa wa fintech 2.0. Tukio hili limefanyika tarehe 2 Aprili 2026, katika makao makuu ya Vodacom Tanzania, jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Teknolojia na Mawasiliano, Vodacom Tanzania Plc, imetangaza kukamilika kwa maboresho makubwa ya huduma ya kifedha kwa njia ya simu, M-Pesa, kufuatia uwekezaji wa kimkakati wa dola za Marekani milioni 28 uliolenga kuimarisha uthabiti, usalama na uzoefu wa wateja katika huduma za kifedha kidijitali nchini.
Akizungumza Aprili 1, 2026 jijini Dar es Salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa Vodacom Tanzania, Philip Besiimire, alisema uwekezaji huo unaweka msingi imara wa mustakabali wa M-Pesa kwa kuhamisha huduma hiyo kutoka mfumo wa awali wa G2 kwenda kwenye mfumo wa kisasa wa teknolojia ya kifedha ulioboreshwa wenye uwezo mkubwa zaidi wa kushughulikia miamala na kutoa huduma kwa ufanisi.
Alisema maboresho hayo yanalenga kuhakikisha M-Pesa inaendelea kuwa huduma salama na ya kuaminika inayoweza kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya watumiaji wa huduma za kifedha kidijitali nchini, huku ikiendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia.
Kwa upande wa wateja, maboresho hayo yanatarajiwa kupunguza changamoto za kukatika kwa huduma, kwani mfumo mpya umeboreshwa kuruhusu matengenezo na maboresho kufanyika ndani ya muda mfupi zaidi, kutoka masaa hadi dakika chache, hali itakayosaidia kuendelea kwa miamala ya kila siku bila usumbufu.
Aidha, Vodacom imesema mfumo huo mpya umeongeza viwango vya usalama katika kulinda taarifa na miamala ya wateja, huku ukiwapa mawakala, wafanyabiashara na washirika wa kibiashara uwezo mkubwa zaidi wa kushughulikia miamala, kupata taarifa za kina na kusimamia huduma kwa uwazi zaidi.
Maboresho hayo pia yatawezesha kuanzishwa kwa huduma mpya kwa urahisi zaidi katika maeneo ya akiba, mikopo, malipo na huduma za biashara, hatua inayotarajiwa kupanua matumizi ya huduma za kifedha kidijitali na kuongeza ujumuishwaji wa kifedha nchini.
Kampuni hiyo imeeleza kuwa sehemu ya utekelezaji wa maboresho hayo ni kipindi maalum cha siku 30 cha huduma mahususi kwa wateja kinachojulikana kama HyperCare, ambapo timu za kiufundi na huduma kwa wateja zitafuatilia kwa karibu mfumo huo ili kushughulikia changamoto zozote zitakazojitokeza na kuhakikisha huduma inaendelea kutolewa bila usumbufu.
Hatua hiyo inaonesha dhamira ya Vodacom Tanzania kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya kidijitali na kuimarisha mageuzi ya teknolojia nchini, huku ikiendeleza nafasi yake katika kukuza ujumuishwaji wa kifedha na fursa za uchumi jumuishi kwa Watanzania.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...