Wakazi wa Mtwara na maeneo ya jirani wanatarajiwa kunufaika na upatikanaji rahisi na wa haraka wa huduma za mawasiliano na kifedha kufuatia uzinduzi wa duka jipya la Yas, hatua itakayorahisisha miamala ya kila siku, kuimarisha biashara ndogondogo, na kuongeza ushiriki katika uchumi wa kidijitali.
Uzinduzi huo umefanywa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Donald Msengi na ni sehemu ya mkakati wa Yas kupanua huduma zake kote nchini ili kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata huduma za kidijitali karibu nao.
Hatua hii inatarajiwa kuwa na manufaa makubwa kwa makundi mbalimbali ya kijamii ikiwemo wafanyabiashara wadogo, wavuvi, wakulima na vijana, ambao hutegemea huduma za kifedha na mawasiliano katika shughuli zao za kila siku.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mhe.Msengi alisema “Uzinduzi wa duka hili ni ishara ya maendeleo kwa Mkoa wetu. Huduma hizi zitachochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi, kuongeza ajira na kurahisisha maisha ya wananchi wetu. Ni hatua muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu karibu yao.”
Kwa upande wake, Mkuu wa Maduka ya Yas Tanzania Bi. Sarah Sonelo, alisema kuwa uamuzi wa kufungua duka hilo umetokana na uhitaji mkubwa wa huduma za uhakika katika ukanda huo wenye shughuli nyingi za kiuchumi.
“Mtwara ni kitovu muhimu cha shughuli za kiuchumi kwa nchi yetu kama kilimo cha korosho, uvuvi, gesi asilia na biashara za bandari. Kupitia duka hili, tunalenga kusogeza huduma karibu zaidi na wateja wetu, kuwawezesha kufanya miamala yao kwa haraka, salama na kwa urahisi, pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi wa eneo hili.”
Aliongeza kuwa duka hilo litatoa huduma mbalimbali za kidijitali na kifedha ikiwemo usajili wa laini, ununuzi wa simu janja na vifaa vya intaneti, pamoja na huduma za kifedha kupitia Mixx kama vile kutuma na kupokea fedha na malipo ya huduma mbalimbali.
“Dhamira yetu ni kuwa mshirika sahihi wa huduma za kidijitali na kifedha kwa kila Mtanzania, na uwekezaji huu unaonesha namna tunavyoendelea kuleta suluhisho zinazogusa maisha ya watu moja kwa moja,” alisisitiza.
Naye Mkurugenzi wa Yas Kanda ya Kusini na Nyanda za Juu Kusini, Bw. Joseph Mutalemwa, alisisitiza kwamba kampuni ya Yas, imeendelea kuwekeza katika kuhakikisha wakazi wa Mtwara na viunga vyake wanapata huduma bora.
“Tunajivunia kuwa kampuni yenye mtandao wenye kasi na mpana zaidi wa 4G na 5G ulioenea nchi nzima, na tunatamani kila mtanzania afaidi huduma zetu, ndio maana tumejipanga kuhakikisha wakazi wa Mtwara wanapata huduma zinazokidhi mahitaji yao ya kila siku.
Duka hili ni fursa ya kupunguza changamoto zozote za kimawasiliano na kifedha na kuwezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kisasa.”
Uzinduzi huu unaongeza idadi ya maduka makubwa ya Yas mkoani Mtwara kuwa mawili pamoja na maduka madogo (14) yote yakiwa ni sehemu ya mtandao mpana wa zaidi ya maduka 500 ya Yas yaliyoenea nchi nzima, hatua inayolenga kuhakikisha kila Mtanzania, bila kujali alipo, anapata fursa sawa ya kunufaika na huduma za kidijitali.








Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...