Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Katika kukabiliana na changamoto kama mabadiliko ya tabianchi na upotevu wa bio-anuai, watafiti nchini wamehimizwa kuhakikisha tafiti zao zinatoa suluhisho la moja kwa moja kwa jamii badala ya kubaki kwenye maandiko ya kitaaluma pekee.

Wito huo umetolewa leo Aprili 1, 2025 na wadau mbalimbali wa sekta ya utafiti wakati wa mkutano wa kuadhimisha miaka 50 ya jarida la Tanzania Journal of Science (TJS) uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Imeelezwa kuwa tafiti za kisayansi zina mchango mkubwa katika kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, hivyo kuna umuhimu wa kuhakikisha matokeo yake yanawafikia wananchi pamoja na watendaji kwa utekelezaji.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi, amesema watafiti wana wajibu wa kuhakikisha tafiti wanazozifanya zinakuwa chachu ya maendeleo ya taifa.

Amebainisha kuwa Tanzania inalenga kufikia uchumi wa dola za Kimarekani trilioni moja ifikapo mwaka 2050, sambamba na kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja kufikia wastani wa dola 7,000 kwa mwaka.

Ameongeza kuwa mafanikio hayo hayawezi kupatikana bila kuongeza tija katika sekta zote za uzalishaji kupitia tafiti zenye manufaa kwa jamii.

Katika hatua nyingine, ametoa tahadhari kwa watafiti na wahariri wa majarida ya kitaaluma kuhusu matumizi yasiyo sahihi ya teknolojia ya Akili Unde (AI), akisema inaweza kutumika vibaya kuzalisha taarifa zisizo za kweli na kuhatarisha uaminifu wa tafiti.

“Watafiti wasiokuwa makini wanaweza kutumia AI kutengeneza taarifa za uongo, jambo ambalo linaweza kuharibu sifa na uaminifu wa majarida ya kisayansi nchini,” amesema.

Kwa upande wake, Mratibu wa mkutano huo, Profesa Andrew Macrice kutoka UDSM, amesema maadhimisho hayo hayalengi tu kusherehekea mafanikio ya miaka 50 iliyopita, bali pia kuweka mikakati madhubuti kwa miaka ijayo.

Ametaja baadhi ya changamoto zinazohitaji tafiti makini kuwa ni pamoja na upotevu wa ardhi, mabadiliko ya tabianchi, uhaba wa chakula na kupungua kwa bio-anuai.

Nae Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye, amesema sayansi inapaswa kushirikiana na jamii na kusaidia katika utungaji wa sera zinazogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.

Amesema kuwa jarida la TJS limekuwa nyenzo muhimu katika kuwajenga watafiti chipukizi na kutoa jukwaa la kubadilishana mawazo ya kitaaluma.

Pamoja na hayo ametoa wito kwa watafiti vijana kutumia fursa ya maadhimisho hayo kama chachu ya kukuza taaluma zao, akisisitiza kuwa mustakabali wa sayansi nchini unategemea nidhamu, uadilifu na ubunifu.

Jarida la TJS, ambalo ni miongoni mwa majarida 27 yanayomilikiwa na UDSM, limeendelea kupata mafanikio kwa kuingia katika mifumo ya kimataifa ya uchapishaji, hatua inayoongeza ushindani na mwonekano wa tafiti za Tanzania duniani.

















Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...