Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeweka wazi mkakati wake wa kuendeleza sekta ya TEHAMA kwa kuwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2026/2027. Bajeti hiyo inalenga kuimarisha miundombinu ya mawasiliano pamoja na kukuza uchumi wa kidijitali nchini.

Akiwasilisha taarifa hiyo, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, amesema wizara inatarajia kukusanya jumla ya Shilingi 160,369,240,000. Mapato hayo yanatarajiwa kutokana na uuzaji wa huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, ambao umeendelea kupanuka na kuongeza matumizi ndani na nje ya mipaka ya nchi.

Amesema kuwa ongezeko la makusanyo linachochewa na kuimarika kwa matumizi ya huduma za mawasiliano, sambamba na juhudi za serikali kueneza miundombinu ya intaneti hadi maeneo zaidi ya vijijini na mijini. Hatua hiyo inalenga kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma bora na za uhakika.

Kwa upande wa matumizi, wizara imeomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi 222,589,451,000 kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake katika mwaka ujao wa fedha. Kiasi hicho kinajumuisha matumizi ya kawaida na fedha za miradi ya maendeleo.

Kati ya fedha hizo, Shilingi 13,146,172,000 sawa na asilimia 5.9 ya bajeti yote zimetengwa kwa matumizi ya kawaida. Ndani ya fungu hilo, Shilingi 6,371,830,000 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi, huku Shilingi 6,774,342,000 zikielekezwa kwenye gharama nyingine za uendeshaji wa wizara.

Sehemu kubwa ya bajeti hiyo, ambayo ni Shilingi 209,443,279,000 sawa na asilimia 94.1, imeelekezwa katika miradi ya maendeleo. Mgawanyo wa fedha hizo unaonesha kuwa Shilingi 98,480,905,000 ni fedha za ndani, wakati Shilingi 110,962,374,000 zitatoka kwa washirika wa maendeleo kutoka nje ya nchi.

Waziri Kairuki amesisisitiza kuwa uwekezaji huu mkubwa utaongeza upatikanaji wa huduma za mawasiliano, kuboresha kasi na ubora wa intaneti, pamoja na kufungua fursa mpya za kiuchumi kupitia teknolojia. Aidha, utawezesha sekta mbalimbali kama elimu, afya na biashara kunufaika zaidi na mapinduzi ya kidijitali.

Kwa ujumla, bajeti hiyo inalenga kuharakisha mageuzi ya kidijitali nchini, kuongeza ufanisi wa huduma za umma, na kuiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya ushindani wa kiteknolojia ndani ya ukanda na kimataifa.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...