Benki ya Exim Tanzania imezindua rasmi tawi lake jipya mkoani Geita, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wateja wa eneo hilo, hususani wanaofanya shughuli ndani ya mnyororo wa thamani wa sekta ya madini pamoja na wakulima, wafanyabiashara wadogo na wa kati.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde pamoja na viongozi wa Serikali, wadau wa sekta ya madini,wakulima na wafanyabiashara mbalimbali.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde alisema:

“Sekta ya madini inaendelea kuwa nguzo muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania. Uwepo wa taasisi za kifedha kama Benki ya Exim hapa Geita utaongeza upatikanaji wa mitaji na kuwawezesha wachimbaji pamoja na wafanyabiashara kuendesha shughuli zao kwa ufanisi zaidi,” alisema.

“Hatua hii inaendana vizuri na jitihada za Serikali kuhakikisha manufaa ya sekta ya madini yanawanufaisha Watanzania wengi zaidi,” aliongeza.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim Tanzania, Bw. Jaffari Matundu alisema tawi hilo jipya linaakisi dhamira ya kimkakati ya benki hiyo ya kusogeza huduma za kifedha karibu na maeneo yenye ukuaji mkubwa wa shughuli za kiuchumi.

“Geita ni kitovu muhimu cha shughuli za kiuchumi kinachoendeshwa na sekta ya madini pamoja na biashara zinazoiunga mkono. Kupitia tawi hili, tunalenga kutoa huduma za kifedha zilizo salama, rahisi kufikiwa na zinazokidhi mahitaji ya wateja wetu, kuanzia wachimbaji wadogo hadi wafanyabiashara wakubwa,” alisema.

Aliongeza kuwa benki hiyo itaendelea kutoa suluhisho za kifedha zinazochochea ukuaji wa biashara na kuongeza ushirikishwaji wa kifedha nchini.

“Wajibu wetu unaenda zaidi ya huduma za benki. Tupo kama mshirika wa muda mrefu katika ukuaji wa biashara na maendeleo ya jamii,” aliongeza.

Kama sehemu ya dhamira yake ya kuisaidia jamii kupitia programu ya Exim Cares, benki hiyo pia ilitoa msaada kwa Hospitali ya Manispaa ya Geita kufuatia changamoto zilizobainika katika utoaji wa huduma za afya ya uzazi, watoto wachanga pamoja na huduma za dharura katika eneo hilo.

Msaada huo unatarajiwa kuimarisha uwezo wa hospitali kutoa huduma kwa wakati, kuboresha mwitikio wa huduma za dharura kwa wagonjwa mahututi, na kuchangia matokeo bora ya afya kwa kina mama, watoto wachanga na jamii ya Geita kwa ujumla.

Akizungumzia msaada huo, Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Benki kwa Wateja Binafsi na wa Kati wa Benki ya Exim Tanzania, Bw. Andrew Lyimo alisema:

“Tunaamini ukuaji wa kifedha lazima uende sambamba na ustawi wa jamii. Mchango huu ni sehemu ya jitihada zetu pana za kuunga mkono huduma muhimu za kijamii na kuboresha maisha ya wananchi.”

Tawi la Geita ni sehemu ya mkakati mpana wa Benki ya Exim wa kupanua uwepo wake katika maeneo muhimu ya kiuchumi nchini Tanzania. Katika safari hii ya ukuaji, benki hiyo imeendelea kuongeza mtandao wake katika maeneo yenye fursa kubwa za biashara, ikiwemo maeneo ya utalii na ukarimu kama Paje Zanzibar, huku ikiendelea kuhakikisha biashara na jamii zinapata huduma za kifedha zinazokidhi mahitaji yao pamoja na huduma za kisasa za kibenki.

Ikiendelea kuimarisha dhamira yake ya kusaidia ukuaji wa biashara, Benki ya Exim imeendelea kuanzisha suluhisho mbalimbali zinazojibu mahitaji yanayobadilika ya watu binafsi na biashara katika sekta tofauti. Kutokana na ongezeko la mahitaji ya huduma za mikopo ya magari na uendeshaji bora wa biashara, hivi karibuni benki hiyo iliingia katika ushirikiano wa kimkakati na Toyota Tanzania Limited unaolenga kurahisisha umiliki wa magari kwa watu binafsi na biashara.

Benki hiyo pia imeendelea kuimarisha huduma zake za ufadhili wa mnyororo wa ugavi(supply chain) ili kusaidia biashara katika sekta mbalimbali kupata mtaji wa uendeshaji na kuongeza ufanisi wa shughuli zao.

Kama sehemu ya shughuli za uzinduzi huo, Exim Bank pia iliandaa chakula cha jioni maalum kwa wateja wake pamoja na wadau mbalimbali wa Geita, kilichotoa fursa ya kujenga mahusiano, kusikiliza maoni ya wateja na kujadili namna benki hiyo inaweza kuendelea kusaidia ukuaji wa biashara zao.

Hatua hii inaonyesha dhamira endelevu ya benki hiyo katika ubunifu, ushirikiano na utoaji wa suluhisho za kifedha zinazokidhi mahitaji yanayoendelea kubadilika ya uchumi wa Tanzania.
Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde (katikati), ambaye alikuwa Mgeni Rasmi, akikata utepe wakati wa hafla ya ufunguzi rasmi wa tawi la Exim Bank Tanzania katika Mkoa wa Geita Region, akiwa pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe. Hashim Komba (wa tatu kutoka kushoto). Pia pichani ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Exim Bank Tanzania, Bw. Jaffari Matundu (wa kwanza kutoka kushoto), pamoja na viongozi wengine wa Serikali na Benki ya Exim katika tukio hilo lilofanyika mnamo tarehe 09 May 2026, Geita.










Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...