Na Seif Mangwangi, Arusha
BENKI ya CRDB, imepongeza taasisi ya Mawakili ya Wakili Welfare Mkoba kwa kupiga hatua kubwa ya uwekezaji hadi kufanikiwa kupata mtaji wa zaidi bilioni moja kwa kipindi kifupi tu cha miaka miwili tangu kuanzishwa kwake.
Aidha imeelezwa kuwa wastaafu wengi wamekuwa wakipoteza maisha kwa muda mfupi mara baada ya kustaafu kufuatia kukosa elimu sahihi ya fursa za kiuchumi zilizopo kwenye uwekezaji na kujikuta wakiwekeza kwenye maeneo yenye mazingira hatarishi ya kibiashara.
Hayo yameelezwa Aprili 29, 2026 Jijini hapa na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Abdulmajid Nsekela katika salamu zake zilizowasilishwa na Kaimu Meneja wa Benki hiyo Kanda ya kaskazini, Emmanuel kafui wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa mwaka wa taasisi ya Mawakili ya Wakili Welfare Mkoba.
Kafui amesema waajiriwa wengi wamekuwa wakipata msongo wa mawazo pale wanapostaafu kufuatia kuwekeza kwenye maeneo yasiyokuwa sahihi na kuwataka kufanya utafiti kwanza kabla ya kujiingiza kwenye biashara pindi wanapostaafu.
Amesema Benki ya CRDB imeanzisha kitengo cha kutoa elimu ya uwekezaji pamoja na fursa za kiuchumi zilizopo na kuwakaribisha watanzania wote kufika kupata elimu hiyo ambayo ni Bure.
Awali akiwasilisha risala ya taasisi ya Wakili Welfare Mkoba, Mwenyekiti wa taasisi hiyo Wakili Laetitia Ntagazwa amesema taasisi hiyo ilianzishwa mwaka 2023 baada ya kubaini kuwepo kwa changamoto mbalimbali za kiuchumi na kijamii zinazowakabili Mawakili nchini.
Letiticia ambaye pia ni Kaimu Rais wa chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), amesema tangu ilipoanzishwa taasisi hiyo yenye wanachama 350 wamefanikiwa kukusanya mtaji wa zaidi ya bilioni moja.
" Kwa miaka miwili tangu tumeanzisha taasisi hii tumeshakusanya mtaji wa bilioni 1.350, ambapo pia tumewekeza kwenye mfuko wa uwekezaji wa UTT kiasi cha milioni400 na kutoa mikopo ya Milioni 840," amesema.
Amesema malengo ya taasisi hiyo Kwa mwaka 2026/2027 ni kukusanya kiasi cha bilioni 2, na kuendelea kutoa mikopo mingi zaidi Kwa Mawakili wanachama Ili kuwajenga kiuchumi na kufurahi maisha.
Letiticia amesema Kwa fedha walizokuwa nazo hivi sasa, Kila mwanachama ana uhakika wa kupata gawio la Milioni 200 Kwa mwaka jambo ambalo linaendelea kuleta faraja Kwa wanachama wake.
Aidha amewataka Mawakili zaidi kujiunga na taasisi hiyo kwa kile alichosema masharti ni rahisi sana na kwamba malengo ya taasisi ni kuwa na Benki yake inayojitegemea.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, CPA Mfaume Mbuma amesema riba ya mkopo wa dharura ambayo wanachama hukatwa ni asilimia 3 huku riba ya mkopo mkubwa kuanzia milioni10 ikiwa ni asilimia 6 pekee.


.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...