Na. Aron Msigwa – Nairobi, Kenya
Maafisa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi, Zimamoto, Magereza, Uhamiaji pamoja na wataalamu kutoka wizara na taasisi mbalimbali za kiraia wanaendelea kushiriki kwa mafanikio Zoezi la 14 la pamoja la vituo vya uamrishaji vya kijeshi vya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki lijulikanalo kama USHIRIKIANO IMARA 2026, linaloendelea katika Kituo cha Mafunzo cha Masuala ya Usalama na Haki za Binadamu (HPSS), jijini Nairobi nchini Kenya.
Tangu kuanza kwa mafunzo hayo, vikosi vya nchi wanachama vinaendelea kushirikiana kwa karibu katika kubadilishana uzoefu wa kijeshi, kuimarisha uwezo wa pamoja wa kiusalama pamoja na kujenga mshikamano wa kikanda katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazotishia amani na utulivu wa Afrika Mashariki.
Mbali na operesheni za ulinzi wa amani, mafunzo hayo pia yanajikita katika kubadilishana mbinu mapambano dhidi ya ugaidi, uharamia wa baharini, usimamizi wa maafa, vitisho vinavyojitokeza pamoja na mbinu za kukabiliana na majanga na changamoto nyingine za kiusalama zinazoweza kuhatarisha usalama wa kikanda.
Katika zoezi hilo, kikosi cha Tanzania kimeendelea kuonesha uwezo mkubwa na taaluma ya hali ya juu katika maeneo mbalimbali ikiwemo mawasiliano ya kimkakati, uratibu wa operesheni, ubadilishanaji wa taarifa za kiusalama, doria za mijini pamoja na utendaji katika mazingira yenye hatari kubwa.
Zoezi hilo la USHIRIKIANO IMARA 2026 linafanyika kwa muda wa wiki mbili chini ya Itifaki ya Ushirikiano wa Masuala ya Ulinzi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, inayolenga kuimarisha mshikamano wa kijeshi na kiraia kupitia upangaji na utekelezaji wa operesheni za pamoja kwa ajili ya kulinda amani, usalama na utulivu wa ukanda wa Afrika Mashariki.
Kikosi cha Tanzania kinachoshiriki zoezi hilo lililozinduliwa rasmi Mei 14 Jijini Nairobi, Kenya kiliagwa rasmi Mei 9, 2026 na Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu, Meja Jenerali Fadhili Omary Nondo kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Jacob John Mkunda, ambaye alimkabidhi Bendera ya Taifa Brigedia Jenerali Maneno Almasi Mabakila kuongoza ujumbe huo nchini Kenya kuungana na vikosi vya kijeshi kutoka Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Somalia, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Msimamizi Mkuu wa zoezi la 14 la pamoja la Vituo vya Uamrishaji vya Kijeshi vya Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki - Ushirikiano Imara 2026, (Chief Umpire) ambaye pia ni Kiongozi wa kikosi cha Tanzania, Brigedia Jenerali Maneno Almasi akitoa maelekezo mbalimbali kwa Maafisa wanaoshiriki zoezi hilo leo Mei 18, 2026 jijini Nairobi, Kenya.
Zoezi hilo kubwa la kijeshi la pamoja limekusanya washiriki kutoka nchi za Kenya, Tanzania, Uganda, Burundi, Rwanda, Sudani Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Somalia kwa lengo la kuimarisha utayari, ushirikiano na uwezo wa vikosi vya ulinzi vya Majeshi, Polisi, Magereza, Uhamiaji, Zimamoto, Wizara na taasisi za kiraia katika kukabiliana na changamoto za kiusalama zinazolikabili eneo la Afrika Mashariki.


.jpeg)



.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...