▪️ Watakiwa kuongeza bidii na kudumisha mshikamano
📍 Dodoma
Watumishi wa Tume ya Madini wameaswa kuzingatia weledi, uwajibikaji na mshikamano katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuendeleza mafanikio ya Tume pamoja na kuongeza mchango wa sekta ya madini katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Akizungumza leo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) yaliyofanyika kimkoa katika Viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Tume ya Madini, Nsajigwa Kabigi, amesema mafanikio yaliyopatikana yanapaswa kulindwa kwa kuongeza bidii, nidhamu na uwajibikaji kazini.
Kabigi amesema Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, amewapongeza watumishi wote wa Tume waliopo Dodoma, wale walioshiriki maadhimisho ya kitaifa mkoani Njombe pamoja na watumishi waliopo katika mikoa mbalimbali ya kimadini nchini kwa juhudi zao katika kutekeleza majukumu ya kazi.
“Tumeaswa kuendelea kudumisha mshikamano, upendo na kufanya kazi kwa bidii ili kuendelea kuiweka Tume ya Madini katika nafasi ya juu ya utendaji,” amesema Kabigi.
Ameeleza kuwa Tume ya Madini imeendelea kufanya vizuri katika utekelezaji wa majukumu yake, akisisitiza kuwa ni wajibu wa kila mtumishi kuhakikisha taasisi inaendelea kuwa kinara katika ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kutoka sekta ya madini.
Aidha, amesema waajiri wataendelea kulinda haki za wafanyakazi mahali pa kazi, huku akisisitiza kuwa watumishi wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na bidii ili kufikia malengo ya sekta ya madini na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
Katika maadhimisho hayo ya Mei Mosi mkoani Dodoma, maandamano ya wafanyakazi yalianzia Viwanja vya Bunge na kuhitimishwa katika Viwanja vya Jamhuri, ambapo yalipokelewa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule.



.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...