KAMATI ya  Bunge ya kudumu ya Bajeti imeipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)kwa kuanzisha kitengo maalumu kwa ajili ya walipakodi wakubwa hatua ambayo imechangia ongezeko la kodi inayokusanywa na mamlaka hiyo.

Aidha Kamati hiyo imewatoa hofu wananchi juu ya dhana ya uwepo wa upendeleo wa kutolipa kodi kwa walipa kodi wakubwa ikisisitiza kuwa kila mwenye wajibu wa kulipa kodi kwa Mamlaka hiyo analipa kulingana na kiwango kile kile anachostahili.

Akizungumza wakati wa ziara ya kamati hiyo kutembelea kitengo cha walipa kodi wakubwa Jijini Dar es Salaam Mei 30, 2026 Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mashimba Ndaki amesema kuboreshwa kwa mazingira  na kufanya kuwa kama 'faragha' kwa mlipa kodi mkubwa kumewavutia wengi na hivyo kufanya mapato kupaa.

"Kwa namna hali ilivyo, ni tofauti na miaka miwili iliyopita, Sasa hivi walipa kodi wakubwa wanachangia asilia 40 ya Kodi tunayoikusanya, hiki ni kiwango kikubwa ambacho msingi wake Mkuu ni kuboreshwa kwa mazingira kulikofanywa na TRA kwa hili tunawapongeza sana" amesema Mashimba.

Pamoja na hilo amesema TRA imepiga hatua kubwa kwa kuboresha huduma mbalimbali ikiwemo ya watumishi wake kuwa na lugha nzuri jambo linalowavutia wananchi wengi kulipa kodi kwa hiari tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo Mamlaka hiyo ilikuwa ikiogopeka.

Kuhusu dhana ya upendeleo kwa walipa kodi wakubwa, Ndaki amesisitiza kuwa hilo siyo jambo la kweli na ndiyo maana walipa kodi hao wameweza kuchangia asilimia 40 ya kodi yote iliyokusanywa huku walipa kodi wengine wakichangia asilimia 60 zilizobaki.

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Yusuph Juma Mwenda ameshukuru hatua ya Kamati ya Bunge kuzitembelea Mamlaka hiyo akidai kuwa ziara hiyo itazidi kuwahamasisha kuendelea kuboresha huduma zao.

Amesema TRA itaendelea kutenda haki kwa walipa kodi wote kwa kuzingatia madaraja yao  kwa yule anastahili kulipa kikubwa atalipa kikubwa, anayestahili kulipa kidogo atalipa kidogo na yule asiyestahili kulipa hatolipa kwa kuwa hiyo ndiyo utaratibu wa utendaji wa Mamlaka hiyo.

Amesema uwepo wa Ofisi hiyo kwa ajili ya walipa kodi wakubwa wakiwemo wenye makampuni mbalimbali zaidi ya 851 ambao wamechangia asilimia 40 sawa na Trilioni 14 ya kodi iliyokusanywa  Mwaka huu ni kielelezo tosha cha kuwa walipa kodi wakubwa wanalipa kodi.




 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...