Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Agness K. Meena, amesema viongozi wanapaswa kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto za watumishi badala ya kuwa chanzo cha hofu kupitia adhabu zisizo na uchunguzi wa kina.
Ametoa kauli hiyo leo Mei 8, 2026 katika Mkutano wa 13 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Wakala ya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) uliofanyika jijini Dodoma.
Amesema Serikali ina matarajio makubwa kwa sekta ya mifugo katika kukuza uchumi wa Taifa, hivyo ni lazima viongozi na watumishi washirikiane kuhakikisha utendaji bora na uwajibikaji unaongezeka.
“Kiongozi mzuri ni yule anayejua changamoto za watumishi wake na kuona namna ya kutafuta suluhisho, si yule anayetoa adhabu bila kufuatilia kwa undani kama mtu anashida au laah, na ikibainika ni makusudi hatua zinapaswa zichukuliwe na sio kutoa adhabu bila uchunguzi.”
Aidha, amewahimiza viongozi kuwapa watumishi fursa za kujifunza kwa vitendo kupitia safari na mafunzo mbalimbali ili kuwajengea uwezo wa kazi na sio kila safari waende wao tu kwani watumishi huwezi wafundisha bila kuwapa kazi.
Akizungumza Mtendaji Mkuu wa LITA, Dkt. Pius Mwambere, ameishukuru Wizara kwa ushirikiano wake huku akiomba kuendelea kwa programu za kuwajengea uwezo wakufunzi pamoja na kuboresha miundombinu ya kampasi za LITA nchini ikiwemo Tengeru ili iweze kuwa Kampasi mama na kuongeza level ya VIII kwenye kozi zinazotolewa.
Kwa upande wa mwakilishi wa wajumbe waliohudhuria mkutano huo, amesema nasaha zilizotolewa na Katibu Mkuu, zitaenda kutoa mwelekeo ambao wanaamini ushauri wataufanyia kazi kwani wamekumbushwa majukumu yao na watafanya kazi kwa weledi na kuzingatia swala la motisha kwa watumishi ili kuongeza Hamasa ya ufanyaji kazi.
Baraza la LITA linaundwa na Kampasi nane ambazo ni chuo cha Mifugo Tengeru, Mpwampwa, Tanga, Mwanza, Songea-Madaba, Temeke, Morogoro pamoja na Kagera, ambapo awali walikuwa wanadahili wanafunzi kuanzia 700 na sasa wanafikia idadi ya wanafunzi elfu 3000.


.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...