Mkoa wa Ruvuma umeendelea kujizolea umaarufu katika sekta ya madini baada ya makaa ya mawe yanayochimbwa katika wilaya za Mbinga, Songea na Nyasa kufungua masoko katika nchi mbalimbali za Afrika na Asia, huku zaidi ya tani milioni 3.6 zikizalishwa mwaka 2024/2025 na kuchochea ajira, biashara na matumizi ya nishati safi.
Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Alphonce Bikulamchi amesema shughuli za utafiti, uchimbaji na uchakataji wa makaa ya mawe zinazofanywa na makampuni pamoja na wadau mbalimbali zimekuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla.
Amesema makaa hayo yenye ubora wa hali ya juu yanatumika katika viwanda vya saruji, usafishaji wa vyuma na shughuli nyingine za viwandani, huku sehemu ya uzalishaji ikipelekwa katika masoko ya Kenya, Uganda, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
“Migodi ya makaa ya mawe ya Ruvuma imeendelea kuvutia wawekezaji kutokana na ubora wa madini hayo, hali iliyosaidia kufungua masoko mapya katika baadhi ya nchi za Asia na Ulaya,” amesema Mhandisi Bikulamchi.
Ameeleza kuwa ukuaji wa sekta hiyo umechangiwa na kuongezeka kwa uwekezaji pamoja na mahitaji ya nishati duniani tangu mwaka 2019/2020, jambo lililoongeza mchango wa sekta ya madini katika mapato ya Serikali na maendeleo ya Mkoa wa Ruvuma.
Katika hatua nyingine, wadau wa makaa ya mawe mkoani humo wameendelea kuunga mkono agenda ya matumizi ya nishati safi kupitia uzalishaji wa mkaa mbadala unaotokana na makaa ya mawe, wakiwemo Mgodi wa Jitegemee uliopo Wilaya ya Mbinga na Kampuni ya Suzlon ya Wilaya ya Songea.
Migodi hiyo imeendelea kuzalisha mkaa wa nishati safi unaotajwa kusaidia kupunguza matumizi ya mkaa wa kawaida unaotokana na ukataji miti, hatua inayochangia uhifadhi wa mazingira na kupunguza uharibifu wa misitu.
Msimamizi wa Mauzo na Uendeshaji wa Mgodi wa Jitegemee, Mark Tarimo amesema kampuni hiyo imetoa zaidi ya ajira 500 kupitia nafasi za kudumu na mikataba ya mwaka mmoja, huku bidhaa zake zikisafirishwa katika nchi za Afrika Mashariki na Falme za Kiarabu (UAE).
Tarimo amesema kampuni hiyo pia imetekeleza miradi mbalimbali ya kijamii ikiwemo ujenzi wa shule katika Kijiji cha Ruanda, zahanati katika Kijiji cha Luhagara pamoja na usambazaji wa majiko ya nishati safi kwa wananchi.
Naye Mkurugenzi wa Mgodi wa Suzlon, Jigar Chandarana amesema mkaa wa nishati safi unaozalishwa na kampuni hiyo ni mbadala wa mkaa wa kawaida kwa kuwa hudumu kwa muda mrefu, ni nafuu kwa matumizi ya nyumbani na husaidia kulinda mazingira dhidi ya uharibifu wa misitu.
Aidha, Mhandisi Bikulamchi amewataka wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kutumia fursa zilizopo katika sekta ya madini mkoani Ruvuma, huku akiwahimiza vijana kushiriki katika shughuli za uchimbaji, usafirishaji na utoaji wa huduma zinazohusiana na sekta hiyo.


.jpeg)






Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...