Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, ameongoza kikao maalumu cha maprofesa wa chuo hicho kikilenga kujadili mbinu za kuimarisha utafiti, ushauri wa kitaaluma pamoja na mchango wa chuo katika maendeleo ya jamii.
Akihutubia kikao hicho, Prof. Mwegoha ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa jukwaa hilo, alisisitiza umuhimu wa kujenga mshikamano miongoni mwa maprofesa na kutumia mafanikio yaliyopo kama chachu ya maendeleo zaidi. Alieleza kuwa jukwaa hilo limekusudiwa kuunda mazingira ya majadiliano ya wazi yatakayosaidia kutathmini mafanikio yaliyopatikana, sambamba na kuweka dira ya pamoja ya maendeleo ya baadaye akisisitiza umuhimu wa kuongeza vyanzo vya mapato ya ndani ya chuo kupitia shughuli za utafiti na ushauri elekezi.
Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof. Hawa Tundui, alieleza kuwa jukwaa hilo ni hatua muhimu katika kujenga utamaduni thabiti wa kitaaluma. Alibainisha kuwa chuo kina maprofesa kamili watano, maprofesa washiriki 29, wahadhiri waandamizi 64 na wahadhiri 62, huku wahadhiri wasaidizi na wasaidizi wa kufundisha wakizidi 300, hali inayoonesha msingi mpana wa kukuza wanataaluma wa baadaye. Aidha, alisisitiza umuhimu wa uanagenzi katika kuwalea wanataaluma chipukizi kwa weledi.
"Maprofesa wanapaswa kuwa vinara wa mabadiliko kwa kuongoza katika uandishi wa kitaaluma, usimamizi wa tafiti na matumizi ya matokeo ya tafiti katika kutatua changamoto za kijamii".Alisisitiza Prof. Tundui
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utafiti, Machapisho na Masomo ya Uzamili, Dkt. Nsubili Isaga, alieleza kuwa jukwaa hilo litaimarisha maeneo muhimu ikiwemo uanagenzi (Mentorship),utafutaji wa rasilimali kupitia miradi ya utafiti na ushauri, pamoja na kuendeleza huduma kwa jamii. Aidha, alibainisha kuwa jukwaa hilo sasa litakuwa likifanyika kila mwaka kama sehemu ya utamaduni wa chuo wa kujipima na kupanga maendeleo ya baadaye.
Katika hatua nyingine mtoa mada Mwalikwa katika jukwaa hilo ambaye pia ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe mstaafu, Prof. Joseph Kuzilwa, alisisitiza kuwa uanagenzi ni jukumu la msingi la uprofesa linalolenga kukuza kizazi kijacho cha wasomi. Alieleza kuwa uanagenzi bora unahitaji mwongozo wa karibu, kushirikishana uzoefu na mifumo imara ya kuwajengea uwezo wanataaluma chipukizi kitaaluma, kwa vitendo na kimaadili.
Aidha, alisisitiza kuwa maprofesa wanapaswa kuchukua nafasi ya kimkakati katika kusimamia na kuendeleza uanagenzi ili kuhakikisha ubora na uendelevu wa taaluma chuoni hapo.
Kupitia jukwaa hilo, msingi imara umewekwa wa kuimarisha mchango wa maprofesa katika utafiti, ubunifu na maendeleo ya chuo, sambamba na kuhakikisha kuwa maarifa yanayotolewa yanachangia moja kwa moja maendeleo ya jamii, chuo na taifa kwa ujumla.
Makamu Mkuu wa Chuo Prof. William Mwegoha akihutubia katika kikao cha Maprofesa wa chuo kikuu Mzumbe cha kuweka mikakati ya kuongeza tafiti na kuchagiza Maendeleo ya Chuo.







Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...