Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Neema Peter Majule, ameibana Serikali akiitaka kueleza mkakati wake wa kuwasaidia wahitimu wa vyuo vikuu kutumia vyeti vyao vya taaluma kama dhamana ya kupata mikopo kwa ajili ya kuanzisha biashara na miradi ya uwekezaji.
Akizungumza bungeni Jijini Dodoma Mei 21, wakati akiuliza swali namba 409 kwa Wizara ya Fedha, Dkt. Majule alisema kuwa sera ya elimu ya juu kwa sasa inalenga kuzalisha wahitimu wanaoweza kujiajiri na pia kuajiri wengine kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo.
Alieleza kuwa vyuo vikuu vingi Duniani vimeanzisha idara za Career Development kwa lengo la kuwaandaa vijana hao kuingia kwenye ulimwengu wa biashara na uwekezaji mkubwa.
Katika swali lake la kwanza, Dkt. Majule alihoji kama Serikali ipo tayari kuwabaini wahitimu wenye ubunifu na uwezo wa kuanzisha miradi mikubwa, na kuwapatia mikopo mikubwa ili waweze kufungua biashara zitakazosaidia kutoa ajira kwa Watanzania wengine.
Aidha katika swali lake la pili, mbunge huyo alihoji kama Serikali ipo tayari kutoa mitaji mikubwa kwa wahitimu watakaotumia vyeti vyao vya taaluma kama dhamana ya mikopo, au kama bado watahitajika kuwa na dhamana nyingine za ziada ili kupata fedha hizo.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Laurent Luswetula, amesema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka mazingira rafiki ya kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia programu mbalimbali ya mikopo yenye masharti nafuu, na tayari Serikali imetoa mabilioni ya fedha kwa ajili ya kuwawezesha vijana kujiajiri na kuanzisha shughuli za kiuchumi.
Hata hivyo, ameeleza kuwa changamoto kubwa iliyopo ni kwamba wahitimu wengi wa vyuo vikuu bado hawana uzoefu wa kutosha katika kuendesha biashara kubwa na uwekezaji wa kiwango kikubwa.
Amesema Serikali inaamini vijana wanapaswa kuanza na biashara ndogo huku wakijengewa uwezo wa ujasiriamali, usimamizi wa biashara na uwekezaji kabla ya kufikia hatua ya kupata mikopo mikubwa.



.jpeg)
.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...