Mbunge wa Jimbo la Katoro, Mhe. Mhandisi Kija Limbu Ntemi, ameiomba Wizara ya Ujenzi kuanza ujenzi wa barabara ya Ushirombo–Katoro yenye urefu wa km 47 kwa kutokea upande wa Katoro, ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo.
Akichangia wakati wa uwasishwaji wa bajeti ya Wizara ya Ujenzi Bungeni, Mhe. Ntemi amesema ujenzi wa barabara hiyo tayari umeanza kwa kutokea Ushirombo, lakini wananchi wa Katoro hususan eneo la Stamico-CCM bado wanateseka sana na vumbi.
“Namuomba Mhe. Waziri achakate ili barabara hii ianze kujengwa pia kwa kutokea Katoro. Wananchi wangu wamechoka na vumbi, hasa pale Stamico-CCM,” alisema Mhe. Ntemi.
Aidha, mbunge huyo ameishukuru Wizara kwa kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Chibingo–Chigunga, akisema hatua hiyo itarahisisha shughuli za kiuchumi na usafirishaji kwa wakazi wa maeneo hayo.
Mhe. Ntemi ameitaka Wizara kuhakikisha inawapata wakandarasi waliobobea na wenye rekodi nzuri ili kuepusha ujenzi wa barabara zisizodumu. Alisema kumekuwa na tabia ya baadhi ya wakandarasi kufanya kazi zisizo na kiwango, na kusababisha barabara kuharibika mara kwa mara.
Katika kueleza umuhimu wa ubora, alitolea mfano barabara ya Kahama–Masumbwe–Ushirombo–Runzewe ambayo amesema imebaki kuwa bora hadi leo licha ya kupitishwa na magari makubwa ya mizigo. “Waziri amtafute huyo mkandarasi aliyejenga barabara hii, ndiye afae kupewa kazi za kujenga barabara za nchi hii,” alishauri.
Vilevile, Mhe. Ntemi alimshukuru Rais wa Awamu ya Sita kwa namna anavyoendelea kufungua barabara mbalimbali nchini, akisema hatua hiyo inachochea maendeleo na kuunganisha mikoa na wilaya kwa urahisi.
Barabara ya Ushirombo–Katoro ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayotarajiwa kufungua fursa za kiuchumi kwa wakazi wa Jimbo la Katoro na maeneo jirani pindi itakapokamilika.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...