Na Said Mwishehe,Michuzi TV

SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan imeendelea kujenga mahusiano mema na nchi jirani zikiwemo za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mahusiano hayo ya Tanzania na nchi jirani yamekuwa ya kihistoria na chini ya uongozi wa Rais Dk.Samia umeweka msingi imara wa kuendeleza ujirani huo hasa ujirani wenye tija kwa nchi hizo.

Ujirani wetu kati ya Tanzania na nchi za jumuiya hiyo umewezesha Mei 3,2026 kushuhudia ujio wa Rais wa Rwanda Paul Kagame na Mei 4 Rais wa Jamhuri ya Kenya Dk.William Ruto .Ni safari za marais wawili tofauti lakini msingi wa safari yao ni muelekeo ule ule wa kujenga uhusiano na ujirani mwema kwa nchi hizo.

Hata hivyo ujio wa Rais Kagame na Rais Rutto pia ni uthibitisho wa nafasi ya Tanzania ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki

Kwa kukumbusha tu nafasi ya Tanzania ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ni pana na ya kimkakati, ikihusisha historia, uchumi, siasa, na usalama wa kikanda. Hapa chini kuna maelezo ya kina yanayokupa picha kamili:

Iko hivi katika historia ya jumuiya hiyo inaonesha Tanzania ni mwanachama mwanzilishi wa EAC (toleo la sasa lililoanzishwa mwaka 2000), pamoja na Kenya na Uganda. Pia ilishiriki katika Jumuiya ya zamani ya Afrika Mashariki iliyovunjika mwaka 1977.

Tanzania imekuwa nguzo ya mshikamano wa kikanda, ikisisitiza ushirikiano wa polepole lakini thabiti (“gradual integration”).Uwepo wa Tanzania umechangia katika kuweka misingi ya sera na taasisi za EAC.

Kwa upande wa kiuchumi Tanzania ina mchango mkubwa katika uchumi wa EAC hasa katika Bandari na Biashara.Katika Bandari ya Dar es Salaam ni lango muhimu kwa biashara ya nchi zisizo na bandari kama Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Pia Tanzania inaunganisha ukanda wa EAC na masoko ya kimataifa kupitia Miundombinu Reli, barabara, na miradi ya nishati husaidia kuunganisha nchi wanachama.

Mfano ni miradi ya reli ya kisasa (SGR) inayolenga kuboresha usafirishaji.Miradi mingine ni Soko la Pamoja ambapo Tanzania ni sehemu ya Soko la Pamoja la EAC (Common Market) – kuruhusu uhuru wa watu, ajira, huduma na mitaji.

Mara nyingi Tanzania imekuwa makini zaidi katika kufungua soko lake kikamilifu ikilinganishwa na baadhi ya wanachama.

Kwa upande wa nafasi ya kisiasa na kidiplomasia Tanzania ina mchango mkubwa katika diplomasia ya kikanda na inajulikana kwa sera ya kutafuta maelewano na amani.Jambo kubwa na la kufurahisha zaidi Tanzania mara nyingi husimama kama mpatanishi muhimu.


Hivyo kwa ujumla, Tanzania ni mhimili wa utulivu, uchumi, na sera za tahadhari ndani ya EAC. Inachangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya jumuiya, huku ikihakikisha maslahi yake ya kitaifa hayapotei katika mchakato wa ujumuishaji wa kikanda.

Nimeeleza kwa kifupi kuhusu nafasi ya Tanzania katika jumuiya hiyo na ujio wa Rais Kagame na Rais Dk.Ruto inaendelea kuthibitisha nafasi na mchango wake kwa nchi hizo.

Hata moja ya mambo ya kuvutia kwa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ni kuona anaendelea kuwa daraja la mahuasiano mema kati yake na nchi jirani. Ile falsafa yake ya 4R imepenya hata katika nchi zinazoizunguka Tanzania.Hizi R4 za Mama zimepenya na kuwa nguzo ya diplomasia, amani na umoja wa Afrika Mashariki

Ikumbukwe katika kipindi cha hivi karibuni, ukanda wa Afrika Mashariki umeshuhudia mijadala mbalimbali ya kisiasa na kijamii iliyovuka mipaka ya nchi moja kwenda nyingine. 

Katika mazingira hayo, falsafa ya “R4 za Mama” imeendelea kujidhihirisha kama dira muhimu ya diplomasia, utulivu na ujenzi wa mahusiano yenye tija kwa taifa na ukanda mzima.

Kwa mtazamo wa wengi, R4 zimeonyesha msimamo wa kulinda heshima, mamlaka na uhuru wa Tanzania bila kuingia katika mvutano usio wa lazima sio tu nchini bali na kwa nchi nyingine za jumuiya ya Afrika Mashariki.

Hii ni kwa sababu taifa lolote huru lina haki ya kuendesha masuala yake ya ndani kwa mujibu wa sheria, taratibu na utashi wa wananchi wake. 

Kauli au matendo yanayoonekana kuingilia uhuru wa nchi nyingine mara nyingi huweza kuathiri mshikamano wa kikanda na kuzua taharuki zisizo za lazima.Ndio maana Rais Dk.Samia anaamini katika maridhiano zaidi .

Hata hivyo, nguvu kubwa ya R4 haipo tu katika kujibu changamoto za kisiasa, bali katika uwezo wake wa kujenga madaraja ya ushirikiano na ujirani mwema. 

Tanzania imeendelea kuonesha diplomasia ya kisasa siyo ya migogoro na majibizano, bali ni ya hekima, mazungumzo na mshikamano wa kikanda. Huo ndio msingi unaoifanya Afrika Mashariki kuendelea kuwa eneo lenye matumaini makubwa ya maendeleo ya pamoja.

Ukanda wa Afrika Mashariki una historia, tamaduni na udugu unaowaunganisha wananchi wake. Mataifa haya yanategemeana katika biashara, uwekezaji, usafirishaji, utalii na hata masuala ya usalama. 

Kwa sababu hiyo, kauli za uchochezi au matusi hazina nafasi katika kujenga mustakabali wa pamoja. Kinachohitajika ni kuheshimiana, kusikilizana na kushirikiana kwa maslahi ya wananchi wa ukanda huu.

Ujio wa Rais Kagame na Rais Rutto ni uthibitisho wa kwamba R4 zimeendelea kuonesha umuhimu wa kudumisha amani na usalama kama msingi wa maendeleo ya kiuchumi. 

Hakuna uchumi imara bila utulivu wa kisiasa, na hakuna ushirikiano wa kweli bila kuheshimu mipaka na mamlaka ya kila taifa. Tanzania, kupitia misingi hiyo, imeendelea kuwa mfano wa nchi inayotanguliza maridhiano, diplomasia na ushirikiano wa kimataifa.

Kwa ujumla, falsafa ya R4 za Mama siyo tu kauli ya kisiasa, bali ni mwelekeo unaolenga kujenga Afrika Mashariki yenye mshikamano, heshima ya mataifa, maendeleo ya pamoja na amani ya kudumu. 

Katika dunia ya leo yenye changamoto nyingi za kisiasa na kiuchumi, diplomasia ya hekima ndiyo silaha muhimu zaidi kuliko mabishano ya mitandaoni au siasa za mgawanyiko.

Wakiwa nchini Tanzania Rais Kagame na Rais Dk.Rutto kila mmoja kwa nafasi yake wamepata nafasi ya kuzungumza na mwenyeji wao Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza mazungumzo yake na Rais Kagame, Rais Dk. Samia alisema Tanzania na Rwanda  zimeendelea kujenga uhusiano wa undugu, ujirani mwema na wa kihistoria, unaoakisi  mshikamano wa muda mrefu kati ya wananchi wa pande zote.

Dk. Samia pia alisema  biashara kati ya Tanzania na Rwanda imeendelea kukua na kufikia thamani ya sh. bilioni 644 mwaka 2025 na kuanzia mwaka 1990 hadi Machi, 2026, Mamlaka ya Uwekezaji Tanzania imesajili miradi 42 ya uwekezaji kutoka Rwanda yenye thamani ya dola za Marekani milioni 325.5, iliyozalisha ajira 2,225 kwa Watanzania.

Pamoja na hatua hiyo, Rais Dk. Samia alisema nchi zote zimekubaliana kuongeza kasi ya kuondoa changamoto za kibiashara, vikiwemo vikwazo visivyo vya kikodi, kupanua biashara na uwekezaji, na kutumia kikamilifu fursa za soko la pamoja la Afrika Mashariki na Soko Huru la Biashara la Afrika.

Kama ilivyokuwa kwa Kagame, ziara ya Rais Dk.Ruto pia imebeba matumaini ya kuimarisha ushirikiano wa kindugu na kimkakati kati ya Tanzania na Kenya katika biashara, uwekezaji, miundombinu, usafirishaji na maeneo mengine ya maslahi ya pamoja.

Ukweli wa mambo ni kwamba Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anastahili pongezi kwa kutekeleza kwa vitendo ahadi ya kujenga diplomasia ya uchumi,siasa na kijamii ambayo mwanzoni kabisa baada ya kuapishwa kushika uongozi wa nchi aliahidi kusimamia na kufanikisha hilo.

Ni wakati wa Watanzania wote kila mmoja kwa nafasi yake kutambua jitihada za Rais Dk.Samia za kuendelea kujenga mahusiano ambayo yanakwenda kufungua fursa mbambali za biashara.

Tunakumbuka wakati Rais Dk.Ruto pamoja na kuelezea masuala mbalimbali yanayohusu nchi hizo hakusita pia Kenya na Tanzania sio tu majirani bali ni ndugu wa kweli ambapo alitoa mifano kadhaa kuthibitisha anachokisema baina ya nchi hizo.

Hata hivyo nimalizie kwa kueleza hivi Tanzania chini ya uongozi mahiri wa Rais Samia iko katika mikono salama na kauli mbiu ya Kazi na Utu tunasonga mbele imekuwa faraja kwa kila mkoja wetu.


Kwa maoni 0713833822/0762451570

Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...