Na Janeth Raphael MichuziTv - Bungeni Dodoma 

Rais wa Kenya, William Ruto, amesema kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Kenya si wa kawaida bali ni wa kipekee na wa kihistoria, uliosimikwa katika misingi ya ujirani wa moja kwa moja, udugu wa kitamaduni na lugha inayowaunganisha wananchi wa mataifa hayo mawili ya Afrika Mashariki.

Akihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma leo, Rais Ruto alieleza kuwa mahusiano kati ya nchi hizo mbili hayawezi kupimwa kwa jicho la kisiasa pekee, bali yanapaswa kueleweka kama uhusiano wa asili uliowekwa na historia na maisha ya kila siku ya wananchi wanaoishi mpakani.

Alisisitiza kuwa Tanzania na Kenya ni majirani wa kudumu waliounganishwa na jiografia na pia uhusiano wa kijamii unaovuka mipaka ya kisiasa, jambo ambalo linapaswa kulindwa na kuendelezwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Ruto alitumia methali maarufu isemayo, “unaweza kuchagua rafiki, lakini jirani unapatiwa na Mungu,” akibainisha kuwa ujirani huo ni zawadi inayopaswa kuendelezwa kwa amani, heshima na ushirikiano wa karibu kati ya mataifa hayo mawili.

Aidha, Rais huyo wa Kenya alieleza kuwa Tanzania na Kenya tayari zinashirikiana kwa kiwango kikubwa katika nyanja mbalimbali za kijamii, kiutamaduni na kiuchumi. Alitaja matumizi ya pamoja ya lugha ya Kiswahili kama mojawapo ya nguzo muhimu inayowaunganisha wananchi wa pande zote mbili.

Pia alizungumzia uwepo wa jamii zinazovuka mipaka ya nchi, kama Wamaasai na Wakuria, ambazo zimeendelea kuimarisha uhusiano wa kifamilia na kitamaduni kati ya Kenya na Tanzania, hivyo kufanya mipaka ya kisiasa isiwe kikwazo cha udugu wao wa muda mrefu.

Ruto aliongeza kuwa mshikamano huo wa asili unapaswa kuwa msingi wa kuimarisha zaidi ushirikiano katika sekta za uchumi, biashara, uwekezaji, elimu na miundombinu ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wake, endapo nchi hizo mbili zitaendeleza mshikamano huo kwa vitendo, wananchi wa Tanzania na Kenya watanufaika moja kwa moja kupitia ongezeko la fursa za ajira, biashara na maendeleo ya kijamii, hatua ambayo itaimarisha zaidi ustawi wa ukanda mzima wa Afrika Mashariki.

Rais Ruto alihitimisha kwa kusisitiza kuwa mustakabali wa mataifa ya Afrika Mashariki upo katika mshikamano, kuondoa vikwazo visivyo vya lazima na kuimarisha ushirikiano unaoweka wananchi mbele kama walengwa wakuu wa maendeleo ya kikanda.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiagana na Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Dkt. William Samoei Ruto mara baada ya kuhitimisha Ziara yake ya Kitaifa, katika viwanja vya Gwaride Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma tarehe 05 Mei, 2026.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...