* Teknolojia ya ndani yafungua soko jipya la bidhaa za nyuki

* Sumu ya nyuki yatumika katika afya, vipodozi na tafiti za dawa

Na Karama Kenyunko

NYUKI ni miongoni mwa wadudu wenye umuhimu mkubwa duniani kutokana na mchango wao katika mazingira, afya ya binadamu na uchumi.

Tofauti na wadudu wengi wa kundi lao, nyuki huzalisha mazao mbalimbali yenye thamani kubwa kama asali, nta, propolis, chavua na sumu ya nyuki.

Ingawa asali na nta zimekuwa maarufu kwa muda mrefu, sumu ya nyuki bado haijafahamika kwa kiwango kikubwa kutokana na ukosefu wa elimu, teknolojia na uwekezaji katika uzalishaji wake.

Hata hivyo, kampuni ya Sensa Tanzania Limited imekuja na ubunifu mpya wa teknolojia ya kuvuna sumu ya nyuki, hatua inayotajwa kufungua ukurasa mpya kwa wafugaji wa nyuki nchini.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Patrick Kitosi, anasema amebuni na kutengeneza mashine maalumu za kuvuna sumu ya nyuki kwa kutumia teknolojia ya umeme na vifaa vya kielektroniki.

Anasema utafiti wa teknolojia hiyo ulianza mwaka 2021 ukiwa na lengo la kuwasaidia wafugaji wa nyuki kutumia fursa ya biashara ya sumu ya nyuki, ambayo ina thamani kubwa katika sekta ya afya na utengenezaji wa dawa.
Kitosi anasema mashine hizo hutumia mawimbi maalumu ya masafa yanayowavuta nyuki kusogea karibu na kifaa hicho.

"Nyuki wanapogusa sehemu ya mashine hupata msisimko mdogo wa umeme unaochochea utoaji wa sumu kama njia ya kujilinda," anasema.

Anaeleza kuwa sumu hiyo hukusanyika kwenye kifaa katika mfumo wa unga, ambapo mfugaji anaweza kuikusanya, kuipima kwa gramu na kuiuza katika masoko mbalimbali.

Kitosi anasema wafugaji wengi wamejikita zaidi kwenye uzalishaji wa asali na nta, huku bidhaa nyingine zinazotokana na nyuki zikiendelea kutofahamika kwa kiwango kikubwa.

"Mbali na asali, nyuki huzalisha pia chavua, gundi ya nyuki, maziwa ya nyuki na sumu ya nyuki, ambazo zote zina soko kubwa ndani na nje ya nchi," anafafanua.

Anaongeza kuwa sumu ya nyuki ina matumizi mbalimbali katika sekta ya afya ikiwemo kusaidia katika utengenezaji wa dawa na tafiti mbalimbali za kitabibu.

Katika sumu hiyo kuna kiambata kinachoitwa apitoxin ambacho tafiti mbalimbali zinaeleza kuwa na uwezo wa kusaidia katika matumizi ya kitabibu, ikiwemo kupunguza baadhi ya maumivu ya viungo na kusaidia tafiti zinazohusiana na matatizo ya mfumo wa neva.

Pia, baadhi ya viambata vilivyopo kwenye sumu hiyo vinaelezwa kuwa na uwezo wa kupambana na bakteria, fangasi na baadhi ya virusi.
Teknolojia Inavyofanya Kazi
Tofauti na njia za zamani ambazo zilikuwa ngumu na wakati mwingine kuathiri nyuki, mashine zilizobuniwa na Sensa Tanzania Limited zinaruhusu sumu kuvunwa bila kuwaua nyuki.

Kwa mujibu wa Kitosi, mzinga mmoja unaweza kutoa kati ya gramu 0.8 hadi 1.5 za sumu ndani ya takribani dakika 30, kutegemeana na idadi ya nyuki waliopo kwenye mzinga huo.

Mashine hizo hutengenezwa kulingana na mahitaji ya mfugaji, ambapo zipo zinazoweza kuvuna mzinga mmoja au mizinga mingi kwa wakati mmoja.

"Bei ya mashine ndogo inaanzia Sh 500,000 na huongezeka kulingana na uwezo wa kifaa. Changamoto kubwa iliyopo ni ukosefu wa elimu kuhusu biashara ya sumu ya nyuki pamoja na uhaba wa teknolojia za kisasa kwa wafugaji wengi nchini," anasema.
Fursa ya Soko la Kimataifa
Kwa mujibu wa Kitosi, masoko makubwa ya sumu ya nyuki yanapatikana katika nchi za India, China na Algeria ambako hutumika zaidi katika viwanda vya dawa.

Hata hivyo, amesema ubora wa sumu ya nyuki hutegemea mazingira pamoja na aina ya mimea ambayo nyuki wameitumia kupata chakula.

Anasema mwaka 2022 kampuni hiyo ilipata msaada wa Sh milioni 28 kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia kupitia mfuko wa sayansi na ubunifu, fedha zilizosaidia kuendeleza tafiti za teknolojia hiyo.

"Sensa Tanzania tunaamini teknolojia inaweza kusaidia kuongeza ajira kwa vijana na kuboresha sekta ya ufugaji wa nyuki nchini kupitia vifaa vinavyotengenezwa hapa Tanzania," anasema.

Ubunifu huo unaendana na Dira ya 2050 inayoweka mkazo katika kukuza uchumi shindani unaotumia maarifa, teknolojia na utafiti kuongeza uzalishaji na thamani ya bidhaa zinazotokana na rasilimali za asili.

Katika muktadha huo, bidhaa za nyuki kama sumu ya nyuki zinaweza kuwa sehemu ya uchumi mpya unaoendelea kukua duniani, huku sekta ya nyuki ikiendelea kuwa muhimu katika usalama wa chakula na uhifadhi wa mazingira.

Nyuki wanapoongeza shughuli za uchavushaji, huchangia kuongeza mavuno ya mazao ya kilimo pamoja na kuhifadhi bioanuwai na miti inayosaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Kampuni hiyo yenye makao yake Magomeni, Dar es Salaam, inaendelea kufanya tafiti za teknolojia nyingine zitakazorahisisha uvunaji wa bidhaa mbalimbali zinazotokana na nyuki.

Naye Mshauri wa masuala ya uvunaji wa mazao ya nyuki, Yassin Masenga, anasema ufugaji wa nyuki una mchango mkubwa katika uhifadhi wa mazingira na uzalishaji wa chakula.

Kwa mujibu wake, nyuki husaidia uchavushaji wa mazao na mimea jambo linaloongeza mavuno kwa wakulima na kusaidia mazingira kuendelea kuwa salama kwa viumbe hai.

"Ufugaji wa nyuki si tu biashara ya asali, bali pia ni sehemu ya kulinda mazingira na kuongeza uzalishaji wa kilimo," anasema.

Masenga anasema sumu ya nyuki imekuwa ikitumika katika baadhi ya tiba za asili na maandalizi ya bidhaa mbalimbali zikiwemo za urembo na matumizi ya kitabibu.

Pia anaonya kuwa matumizi ya sumu hiyo yanahitaji tahadhari kwani hayapendekezwi kwa watu wenye matatizo makubwa ya mzio, upungufu wa damu au baadhi ya changamoto za kiafya.

Kwa upande wake, Ofisa Misitu Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo, Dk Siima Bakengesa, anasema wanakaribisha bunifu zote zinazosaidia kuongeza thamani ya mnyororo mzima wa mazao ya nyuki kwa kuwa zinaweza kusaidia kuinua maisha ya wafugaji.

"Tunaamini kila ubunifu umepitia hatua mbalimbali kabla ya kuanza kutumika. Ndiyo maana tumekuja na Mpango Maalum wa Ufugaji kwa Tanzania iliyobora 2025 ili kuhakikisha bunifu zinazochangia maendeleo zinawafikia Watanzania hususan vijana na wanawake," anasema Dk Bakengesa.

Anasisitiza kuwa nyuki hutoa mazao mbalimbali ikiwemo asali, chavua, nta na sumu ya nyuki ambayo inaendelea kuvutia tafiti na matumizi mbalimbali.

Kadiri elimu, teknolojia na uwekezaji vinavyoendelea kuongezeka, sekta ya nyuki nchini inaweza kutoka kuwa chanzo cha asali pekee na kuwa kitovu kipya cha bidhaa zenye thamani kubwa katika uchumi wa Tanzania.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...