Jumuiya ya wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wa madini ya Metali Tanzania (TBMA) umesema umeanza kuona mafanikio katika kutatua changamoto zinazowakabili wachimbaji wadogo wa madini nchini ikiwemo masoko, viwanda vya uchenjuaji pamoja na kuongeza mapato ya Serikali kupitia sekta ya madini.
Akizungumza Mei 18, 2026 katika Mkutano Mkuu wa Pili wa wanachama wa TBMA uliofanyika Jijini Dodoma, Mwenyekiti wa jumuiya hiyo Thobias Kente amesema wamefanikiwa kuimarisha umoja wa wachimbaji na kuwaunganisha na wenye viwanda vya uchenjuaji wa madini ili kuongeza thamani ya madini.
Kente amesema lengo kuu la jumuiya hiyo ni kuhakikisha utajiri wa madini unawanufaisha wananchi hususan wachimbaji wadogo kwa kuboresha maisha yao kupitia mapato yatokanayo na shughuli za uchimbaji na biashara ya madini.
Amesema kwa sasa wachimbaji wadogo wameanza kupata nafasi kubwa zaidi ya kushiriki katika uchumi wa nchi kupitia sekta ya madini kutokana na juhudi za Serikali na ushirikiano uliopo kati ya wadau wa sekta hiyo.
Kwa upande wake, Katibu wa TBMA, Nobert Kaijage amesema jumuiya hiyo ilisajiliwa mwaka 2024 kwa lengo la kuwa daraja kati ya Serikali na wachimbaji pamoja na kuongeza fursa za uwekezaji na ajira kwa wanachama wake.
Amesema TBMA imeendelea kutoa elimu na ushauri kuhusu uchimbaji salama wa madini huku ikiwa na mpango wa kuwawezesha wachimbaji kupata vifaa vya kisasa kupitia ushirikiano na wadau mbalimbali wa sekta hiyo.
Kaijage amesema mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na ongezeko la wanachama hai kutoka 15 hadi 40 pamoja na kuongezeka kwa uelewa wa sheria, kanuni na miongozo ya sekta ya madini kwa wanachama wa jumuiya hiyo.
Aidha amesema mapato ya jumuiya yameongezeka kupitia michango na ada za wanachama huku TBMA ikiendelea kusaidia utatuzi wa changamoto na migogoro ya wachimbaji katika maeneo mbalimbali ikiwemo Kagera, Dodoma na Lindi.
Amesema kupitia jumuiya hiyo wachimbaji wengi wameanza kupata taarifa muhimu kuhusu masoko ya madini, uwekezaji na taratibu za kisheria jambo ambalo limeongeza uelewa na ushiriki wao katika shughuli za madini.
Hata hivyo amesema wachimbaji bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ucheleweshaji wa vibali vya mazingira na kemikali kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali pamoja na mabadiliko ya bei za madini bila taarifa rasmi.
Ameongeza kuwa baadhi ya wanachama wanashindwa kumudu gharama za utafiti wa madini huku baadhi ya viwanda vikishindwa kununua malighafi kwa bei rafiki jambo linaloathiri uzalishaji na biashara ya madini nchini.
Kaijage amesema ucheleweshaji wa majibu ya changamoto kutoka kwa mamlaka husika umekuwa ukiwasababishia hasara wachimbaji wadogo na kupunguza kasi ya maendeleo ya shughuli zao.
Aidha amesema TBMA inaendelea kuiomba Serikali kuweka mazingira bora zaidi yatakayorahisisha upatikanaji wa vibali na kuongeza ushirikiano kati ya wachimbaji na taasisi za Serikali.
Amesema mipango ya jumuiya hiyo ni kuongeza wanachama wapya kupitia ziara, semina na makongamano pamoja na kuwezesha uanzishwaji wa viwanda vya uchenjuaji wa madini ili kuongeza thamani ya madini yanayochimbwa nchini.
Kaijage amesema jumuiya hiyo itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Serikali pamoja na wadau wengine wa sekta ya madini ili kuhakikisha wachimbaji wadogo wananufaika zaidi na rasilimali za madini zilizopo nchini.



.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...