Na Ashura Mohamed, Karatu
Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) imeridhishwa na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa Mradi wa Utafiti wa Mafuta na Gesi wa Eyasi-Wembere uliopo Wilaya ya Karatu, Mkoa wa Arusha.
Ziara hiyo ya ukaguzi iliongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya TPDC, Balozi Ombeni Sefue, ambaye alisema shirika limepiga hatua kubwa kwa kuhakikisha kazi nyingi za kitaalamu sasa zinafanywa na wataalamu na wakandarasi wazawa wa Kitanzania.
Kwa mujibu wa Balozi Sefue, awali baadhi ya kazi hizo zilikuwa zikifanywa na makampuni ya nje ya nchi, lakini sasa TPDC imeweka mkazo kwa wazawa ili kujenga uwezo wa kitaalamu ndani ya nchi.
“Kazi nyingi za kitaalamu sasa zinafanywa na vijana waliopo hapa nchini kwa ubora unaotakiwa ikiwa ni pamoja na wakandarasi wazawa ambao wameajiriwa na TPDC,” alisema Balozi Sefue.
Akizungumzia matumizi ya fedha katika mradi huo, Balozi Sefue alibainisha kuwa hadi sasa zaidi ya shilingi bilioni 47 zimetumika tangu mradi uanze mwaka 2015 hadi mwaka 2026. Alifafanua kuwa fedha hizo zimetoka ndani ya TPDC, kutokana na imani kuwa utafiti huo utatoa matokeo chanya yatakayonufaisha taifa.
“Sasa utafutaji wa mafuta una hatua nyingi kwa sababu ni gharama kubwa sana kuchimba visima vya mafuta. Huwezi kuanza kuchimba kabla ya kufanya hatua ya kwanza ikakupa matumaini, halafu unaenda hatua ya pili na ya tatu mpaka mwisho unachimba kisima cha majaribio ili kupata matokeo chanya,” alieleza.
Balozi Sefue alitaja changamoto zinazokabili mradi huo kuwa ni pamoja na eneo la Ziwa Eyasi kuwa na tope na wakati mwingine ziwa kuka, hali inayochelewesha utekelezaji wa kazi licha ya mkandarasi kuwa na vifaa vya kisasa.
Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa Eyasi-Wembere, kutoka TPDC,Sindi Maduhu, alisema sasa mradi upo katika hatua ya kuchukua data za mitetemo na wanatarajia kukamilisha awamu ya kwanza ifikapo mwezi Juni 2026.
Aliongeza kuwa kazi hiyo inatekelezwa na mkandarasi mzawa, Kampuni ya African Geophysical Service (AGS), ambayo imepata mafanikio makubwa kutokana na matumizi ya wataalamu wenye ujuzi na mitambo ya kisasa inayolingana na mazingira ya eneo hilo.
Mradi wa Eyasi-Wembere unapitiwa pia na bomba la mafuta la Afrika Mashariki (EACOP), jambo linalotarajiwa kuwezesha usafirishaji wa mafuta yatakayopatikana na kuongeza kasi ya shughuli za utafiti katika eneo hilo.


.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...