Wafugaji nchini wametakiwa kuachana na mbinu za jadi za ufugaji ambazo zimepitwa na wakati na badala yake kutumia teknolojia za kisasa za kidigitali zinazorahisisha usimamizi na ufuatiliaji wa mifugo kuanzia inapozaliwa hadi hatua ya kuchinjwa.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Climb Up Limited, Emmanuel Ngallah, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Maonyesho ya Mifugo Kanda ya Ziwa Mei 30, 2026, mkoani Shinyanga.

Ngallah alisema matumizi ya mifumo ya kidigitali katika sekta ya mifugo yanawawezesha wafugaji kupata taarifa sahihi kuhusu afya, ukuaji na historia ya mifugo yao, jambo linaloongeza tija na thamani ya biashara ya mifugo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Agnes Meena mgeni rasmi katika maonyesho hayo, alisisitiza umuhimu wa wafugaji kuendana na mabadiliko ya teknolojia ili kuongeza uzalishaji na kuifanya sekta ya mifugo kuwa na mchango mkubwa zaidi katika uchumi wa nchi.

Alieleza kuwa serikali inaendelea kuhamasisha matumizi ya teknolojia katika ufugaji ili kuboresha usimamizi wa mifugo, kuongeza ubora wa bidhaa zinazotokana na mifugo na kufungua fursa zaidi za masoko ya ndani na nje ya nchi.

Wakati huo huo, baadhi ya wananchi waliotembelea banda la Climb Up Limited katika maonesho hayo wameeleza kufurahishwa na elimu waliyoipata kuhusu ufugaji wa kisasa na matumizi ya mifumo ya kidigitali.

Wamesema maarifa hayo yatawasaidia kuboresha shughuli zao za ufugaji, kuongeza uzalishaji na kufuatilia kwa urahisi maendeleo ya mifugo yao kwa kutumia teknolojia.

Maonesho ya Mifugo Kanda ya Ziwa yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wadau wa sekta ya mifugo, kampuni za teknolojia na wafugaji kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuhamasisha matumizi ya mbinu za kisasa katika uzalishaji wa mifugo.





 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...