Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Tanzania limesaini Hati za Makubaliano (MoUs) na taasisi 10 za elimu ya juu nchini kwa lengo la kuimarisha ajira kwa wahitimu, maendeleo ya ujuzi wa vitendo, ubunifu pamoja na kuwaandaa vijana kwa soko la ajira.

Makubaliano hayo yamesainiwa Mei 29, 2026 jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano kati ya UNDP Tanzania na taasisi za elimu ya juu kupitia programu za wanafunzi, ubunifu, majadiliano ya kimkakati pamoja na ushirikishwaji wa taasisi mbalimbali.

Ushirikiano huo unatekelezwa kupitia Programu ya Maendeleo ya Vipaji kwa Vijana ya UNDP (UNDP Young Talent Development Programme), inayolenga kuunganisha vyuo vikuu, taasisi za maendeleo pamoja na sekta binafsi katika kusaidia mafunzo ya vitendo, ubunifu, ushauri wa kitaalamu na maandalizi ya ajira kwa wanafunzi na wahitimu vijana.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini   makubaliano hayo, Mwakilishi Mkazi wa UNDP Tanzania,  Shigeki  Komatsubara  alisema ushirikiano huo unaonesha dhamira ya pamoja ya kuwaandaa vijana kwa dunia inayobadilika kwa kasi.

“Mpito kutoka chuoni kwenda katika maisha ya kazi haupaswi kuachiwa bahati nasibu. Vijana wanapaswa kuhitimu sio tu wakiwa na vyeti, bali pia wakiwa na uzoefu, uelewa na mwelekeo wa maisha yao ya baadaye,” alisema.

Kwa upande wake, Naibu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu katika Taasisi ya Uhasibu Arusha (IAA), alisema ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano kati ya vyuo vikuu na fursa kwa vijana.

“Vyuo vikuu vinaweza kutoa elimu ya darasani, lakini ushirikiano wa namna hii unasaidia kuwaunganisha wanafunzi na uzoefu wa vitendo, ushauri wa kitaalamu pamoja na fursa mbalimbali zinazowasaidia kujiandaa kwa maisha ya baadaye,” alisema.

Mpango huo unatarajiwa pia kuziwezesha taasisi za elimu ya juu kuwa sehemu muhimu katika kuchangia agenda ya maendeleo ya Tanzania kupitia ubunifu, tafiti, uongozi wa vijana na utoaji wa suluhisho kwa changamoto za maendeleo ya taifa.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...