Na Mwandishi Wetu, Dodoma

SERIKALI imeanza kuvuna matokeo ya mageuzi ya kidijitali katika sekta ya habari baada ya Waandishi wa Habari 3,357 kuthibitishwa na kupatiwa ithibati ndani ya kipindi cha chini ya mwaka mmoja kupitia mfumo wa kisasa wa TAI HABARI.

Mafanikio hayo ni hatua kubwa katika kuimarisha weledi, uwajibikaji na usimamizi wa taaluma ya uandishi wa habari nchini, kwa kuwa kwa mara ya kwanza sekta hiyo imeanza kuwa na mfumo rasmi, wa kidijitali na unaowezesha kuchakata maombi na kuhakiki waandishi wanaokidhi vigezo kwa mujibu wa sheria ya Huduma za Habari.

Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni jijini Dodoma, Waziri wa wizara hiyo, Mhe. Paul Christian Makonda, alisema kuanzia Julai 2025 hadi Aprili 2026, Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imepokea na kushughulikia jumla ya maombi 4,139 ya usajili kupitia mfumo huo wa TAI HABARI.

Kati ya maombi hayo, Waandishi wa Habari 3,357 waliokidhi vigezo vilivyoainishwa kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229, wamepatiwa ithibati.

Katika hatua nyingine, Waziri Makonda alisema JAB imeshughulikia malalamiko 14 ya uvunjifu wa maadili ya taaluma ya habari, jambo linaloonesha kuanza kuimarika kwa mfumo wa uwajibikaji katika sekta hiyo.

Aidha, Mheshimiwa Makonda alisema Serikali kupitia JAB imeandaa mwongozo maalumu wa kisheria utakaowawezesha Waandishi wa Habari wakongwe walioathiriwa na mfumo wa ithibati kureiea katika mfumo rasmi, kwa kuzingatia masharti ya Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229 ambayo ilitungwa kwa ajili ya kukuza taaluma ya uandishi wa habari.

Alisema kuwa sheria hiyo ilitungwa kwa ajili ya kukuza taaluma ya uandishi wa habari kwa kuweka mfumo wa kitaasis utakaosimamia sekta ya habari. 

“Mwongozo huu unaweka utaratibu wa kisheria wa kutambua na kuthibitisha umahiri wao kupitia tathmini maalumu ya uzoefu, weledi na maadili ya taaluma, na kuwawezesha kupata ithibati kwa mujibu wa sheria.” Alisema Mhe. Makonda

Hatua hii inalenga kulinda taaluma ya uandishi wa habari kwa kuhakikisha hata waandishi wa habari wenye uzoefu mkubwa wanapata nafasi ya kuingia katika mfumo rasmi unaotambuliwa kisheria.












Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...