Na Janeth Raphael -MichuziTv Bungenin Dodoma
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Paschal Katambi Patrobass ameainisha vipaumbele nane (8) vitakavyotekelezwa na Wizara hiyo katika mwaka wa fedha 2026/27, vikilenga kuimarisha usalama wa raia, kuboresha utendaji wa vyombo vya usalama na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akizungumza wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara, Katambi amesema Serikali imejipanga kuendeleza mageuzi makubwa katika sekta ya usalama kwa kuzingatia mahitaji ya sasa ya kiutendaji na mabadiliko ya kiteknolojia.
Vipaumbele 8 vya Wizara 2026/27
Waziri Katambi ameeleza maeneo hayo ya kipaumbele kuwa ni:
1.Uboreshaji wa miundombinu ya vyombo vya usalama
Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya vyombo vya usalama chini ya Wizara, ikiwemo ujenzi na ukarabati wa makazi ya maafisa, wakaguzi, askari na watumishi wasio askari ili kuongeza ufanisi kazini.
2. Upatikanaji wa vitendea kazi
Kipaumbele kingine ni kuboresha upatikanaji wa vitendea kazi, hususan vyombo vya usafiri na usafirishaji kwa vyombo vya usalama ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya kila siku.
3. Utafiti wa kiusalama
Wizara itaendelea kufanya tafiti mbalimbali kubaini sababu za makosa mapya ya jinai na kuweka mikakati madhubuti ya kuyakabili mapema.
4. Uimarishaji wa TEHAMA
Matumizi ya TEHAMA yataendelea kuimarishwa katika huduma zote zinazotolewa na Wizara na taasisi zake ili kuongeza ufanisi, uwazi na kasi ya huduma.
5. Mafunzo kwa watumishi na askari
Serikali itaendelea kuwajengea uwezo watumishi na askari kupitia mafunzo mbalimbali yanayolenga kuongeza weledi na ubora wa utekelezaji wa majukumu yao.
6. Miradi ya ujenzi wa NIDA
Wizara kupitia NIDA inatarajia kuanza ujenzi wa Makao Makuu yake jijini Dodoma, pamoja na ofisi 31 za usajili za wilaya na kituo cha mafunzo na matengenezo ya vifaa vya TEHAMA Kibaha.
7. Makazi ya waathirika wa usafirishaji haramu wa binadamu
Serikali pia itaanza ujenzi wa nyumba salama kwa ajili ya waathirika wa usafirishaji haramu wa binadamu jijini Dar es Salaam, ikiwa ni hatua ya kulinda haki na ustawi wa wahanga.
8. Uimarishaji wa shughuli za uzalishaji mali
Wizara itaendelea kuimarisha shughuli za uzalishaji mali kupitia kilimo, mifugo na viwanda, sambamba na kulinda na kuhifadhi mazingira.


.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...