- zaidi ya Sh milioni 126 zaokolewa katika kipindi cha miezi sita
- huduma za upatikanaji wa hewa tiba zaimarika katika hospitali ya mawenzi
- Zaidi ya Mitungi 3000 ya Oksijeni imezalishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi katika kipindi cha miezi sita tangu mradi huo uanze kufanya kazi , hali iliyosaidia kuondoa changamoto ya upatikanaji wa hewa tiba katika hospitali hiyo.
Hayo yamebainishwa leo na Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Abdillah Issah alipokuwa akisoma taarifa ya ya mradi huo mbele ya Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi alipotembelea na kukagua mradi huo.
Akizungumza baada ya kusomewa taarifa ya mradi na kutembelea sehemu mbalimbali za mradi huo Kihongosi amesema mradi huo ni miongoni mwa uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Kilimanjaro na maeneo jirani.
Kihongosi amesema kabla ya kusimikwa kwa mtambo huo hospitali ilikuwa ikikabiliwa na gharama kubwa za ununuzi na usafirishaji wa oksijeni kutoka nje ya mkoa, hali iliyokuwa ikiathiri ufanisi wa utoaji wa huduma.
“Kupitia uwekezaji huo, hospitali imefanikiwa kupunguza gharama za uendeshaji, kuimarisha huduma za wagonjwa mahututi na kuongeza uwezo wa kusambaza oksijeni katika vituo vingine vinavyohitaji huduma hiyo,” amesema kihongosi.
Katika hatua nyingine amewapongeza viongozi na watumishi wa hospitali hiyo kwa usimamizi mzuri wa huduma, akisisitiza mafanikio hayo yanaonesha namna serikali inavyoendelea kuboresha sekta ya afya na kusogeza huduma bora karibu na wananchi.
Awali akisoma taarifa ya mradi huo Dk Issah amesema mradi huo umegharimu jumla ya Sh bilioni 1.94 na katika kipindi cha miezi sita tangu mradi kuanza kufanya kazi mitungi 3,313 ya Oksijeni imezalishwa katika hospitali hiyo, hali iliyisaidia kuondoa changamoto ya upatikanaji wa hewa tiba.
Pia ameongeza kuwa hatua hiyo imesaidia hospitali hiyo kuokoa takribani Sh milioni 126 katika kipindi cha miezi sita baada ya kuanza kutumia mtambo wa kuzalisha hewa tiba ya oksijeni.
“Hatua hiyo imepunguza utegemezi wa ununuzi wa oksijeni kutoka kwa wazabuni wa nje na kuimarisha utoaji wa huduma za afya katika hospitali ya Mawenzi,” amesema Dk Issah.


.jpeg)


.jpeg)


.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...