
Na GULATONE MASIGA
Katika zama za teknolojia na mawasiliano ya kidijitali, mitandao ya kijamii imekuwa sehemu muhimu ya maisha yetu ya kila siku. Kupitia majukwaa mbalimbali, wananchi wanapata habari, wanabadilishana mawazo, wanafanya biashara, wanajifunza na hata kushiriki katika mijadala ya masuala ya kitaifa na kimataifa.
Hata hivyo, pamoja na manufaa hayo makubwa, mitandao ya kijamii imegeuka kuwa chombo kinachoweza kutumika vibaya kueneza chuki, taarifa za uongo, uchochezi na hamasa zinazoweza kuhatarisha amani na utulivu wa jamii.
Kwa siku za karibuni, Tanzania imeshuhudia kampeni na hamasa kubwa katika baadhi ya mitandao ya kijamii zinazohamasisha vurugu, ghasia na uvunjifu wa sheria kwa madai ya kudai haki au kuonyesha kutoridhika na hali fulani za kisiasa na kijamii.
Wakati haki ya kutoa maoni ni msingi muhimu wa demokrasia, ni lazima kutofautisha kati ya maoni yenye kujenga na uchochezi unaoweza kusababisha madhara kwa taifa zima.
Somo Kutoka Kumbukumbu za Oktoba 2025
Watanzania wengi bado wanakumbuka yaliyotokea mwezi Oktoba 2025. Kilichoanza kama kampeni na hamasa katika mitandao ya kijamii kiligeuka kuwa hali iliyosababisha taharuki, hofu na maumivu kwa sehemu mbalimbali za nchi.
Kulishuhudiwa matukio ya vifo na majeruhi. Miundombinu ya umma iliharibiwa na kuchomwa moto. Baadhi ya biashara na mali binafsi ziliporwa au kuharibiwa. Usafiri ulitatizika katika maeneo mbalimbali, huku wananchi wa kawaida wakibeba mzigo mkubwa wa madhara yaliyotokana na yaliyoitwa maandamano ya amani.
Athari zake hazikuishia kwa waliohusika moja kwa moja pekee. Wafanyabiashara walipoteza mitaji yao. Wanafunzi walikosa utulivu wa kujifunza. Wawekezaji walipata wasiwasi kuhusu mazingira ya biashara. Familia nyingi ziliishi katika hofu na sintofahamu.
Haya ni maumivu ambayo hayapaswi kusahaulika kwa urahisi.
Ukweli Mchungu wa Mitandao ya Kijamii
Moja ya mambo yanayopaswa kutafakariwa kwa kina ni kwamba sehemu kubwa ya wanaohamasisha vurugu na machafuko hawapo maeneo ambayo matukio hayo yanatokea. Wengine wako maelfu ya kilomita mbali katika nchi za Ulaya, Marekani au maeneo mengine duniani.
Wao hawatakutana na moshi wa matairi yanayowaka. Hawatapoteza biashara zao. Hawatakuwa kwenye foleni za dharura hospitalini. Hawatapoteza ajira wala kuhangaika na usafiri au kutafuta chakula kwa sababu shughuli za kiuchumi zimesimama.
Mara nyingi, anayepata madhara ni mwananchi wa kawaida. Ni mama lishe anayekosa wateja. Ni dereva anayekosa safari. Ni mfanyabiashara anayepoteza mtaji wake. Ni mwanafunzi anayekosa masomo. Ni taifa lote linalopoteza muda na rasilimali ambazo zingeelekezwa katika maendeleo mengine zinatumika kujenga upya miundombinu iliyoharibiwa na kuhudumia waathirika.
Ndiyo maana ni muhimu kila Mtanzania kutambua kuwa si kila ujumbe unaosambaa mtandaoni unapaswa kufuatwa bila kuhoji. Elimu ya kidijitali inahitaji uwezo wa kuchambua taarifa, kutambua propaganda, na kupima matokeo ya kile kinachohamasishwa.
Amani ni Mtaji wa Maendeleo
Tanzania imejijengea sifa ya kuwa taifa la amani, umoja na mshikamano kwa miongo mingi. Hii si bahati mbaya. Ni matokeo ya juhudi za viongozi, taasisi na wananchi waliotanguliza maslahi ya taifa mbele ya tofauti zao.
Amani ndiyo imewezesha uwekezaji katika sekta mbalimbali. Ndiyo imewezesha ujenzi wa shule, hospitali, barabara, miradi ya maji na umeme. Ndiyo imewezesha biashara kukua na vijana kupata fursa za ajira.
Historia inaonesha kuwa pale ambapo amani inapotoweka, maendeleo husimama. Wawekezaji huondoka. Uchumi hudorora. Huduma za kijamii huathirika. Mwisho wa siku, gharama hulipwa na wananchi wenyewe.
Kwa sababu hiyo, amani si jambo la kuchukuliwa kawaida. Ni rasilimali ya taifa inayohitaji kulindwa kila siku.
Matumizi Chanya ya Mitandao ya Kijamii
Badala ya kutumia mitandao ya kijamii kueneza chuki, vurugu au taharuki, kuna fursa kubwa zaidi za kuitumia kwa manufaa ya jamii.
Vijana wanaweza kuitumia kujifunza ujuzi mpya, kutangaza biashara zao, kutafuta masoko, kuhamasisha shughuli za maendeleo na kujenga mitandao ya kitaaluma.
Wananchi wanaweza kuitumia kutoa maoni kwa staha, kuibua changamoto za jamii na kushiriki katika mijadala yenye kujenga suluhisho.
Mitandao ya kijamii inaweza kuwa daraja la maendeleo au chanzo cha migogoro. Mwelekeo wake unategemea namna tunavyoichagua kuitumia.
Wajibu wa Kila Mtanzania
Katika kipindi hiki ambacho taarifa husambaa kwa kasi kubwa, kila Mtanzania ana wajibu wa kuwa mlinzi wa amani.
Tusisambaze taarifa ambazo hatujazithibitisha. Tusikubali kutumiwa kama vyombo vya kueneza chuki au uchochezi. Tujiulize kila mara: Je, ujumbe ninaoshiriki kuusambaza unajenga au unabomoa? Unaleta suluhisho au unachochea mgogoro?
Tofauti za maoni ni sehemu ya jamii yoyote ya kidemokrasia. Lakini tofauti hizo zinapaswa kushughulikiwa kwa njia za kistaarabu, za kisheria na zinazolinda maisha na mali za wananchi.
Hitimisho
Watanzania walipata somo kubwa kutokana na matukio ya Oktoba 2025. Somo hilo linapaswa kutukumbusha kuwa amani ikivurugika, hakuna anayebaki salama. Madhara yake huwagusa wote bila kujali itikadi, dini, kabila au hali ya kiuchumi.
Tusikubali tena kuingia katika mkumbo wa hamasa zinazoweza kusababisha machafuko, vurugu na uharibifu. Badala yake, tuutumie uwezo wa teknolojia na mitandao ya kijamii kujenga uchumi, kuimarisha umoja wa kitaifa, kuitangaza Nchi yetu kwa uzuri wake na kuharakisha maendeleo ya nchi yetu.
Amani ya Tanzania ni wajibu wa kila Mtanzania. Tukiilinda leo, tutakuwa tumelinda ustawi wa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Kwa Maoni Na Ushauri
0768497974


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...