Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imezindua kampeni maalum inayofahamika kama “Tunakuona Mbali”, ikiwa ni sehemu ya jitihada zake za kuwawezesha Watanzania kutoka makundi mbalimbali ya kijamii kufikia malengo yao ya maendeleo kupitia huduma rasmi za kifedha.

Kampeni hiyo inalenga kuhamasisha utamaduni wa kuweka akiba, kuwekeza, kutumia huduma za kifedha kwa usahihi na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu fursa zinazotolewa na benki katika kuboresha maisha yao. Kupitia kampeni hiyo, NBC inalenga kuwafikia wafanyakazi, wakulima, watoto, vijana, wanafunzi, wanawake, wastaafu, vikundi vya kijamii, taasisi za dini, Watanzania wanaoishi nje ya nchi pamoja na wafanyabiashara wadogo, wakati, na wakubwa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika katika makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam mapema leo, Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa NBC, Bw. David Raymond, alisema kampeni hiyo imejengwa juu ya falsafa ya kutambua na kuunga mkono ndoto na juhudi za Watanzania katika hatua mbalimbali za maisha yao.

“Tunaposema ‘NBC Tunakuona Mbali’, tunamaanisha kuwa tunakupa zaidi ya huduma za kawaida za benki. Tunatambua kwamba kila Mtanzania ana ndoto na malengo ya kufikia mafanikio katika maisha yake; iwe ni kujenga nyumba, kukuza biashara, kusomesha watoto, kuanzisha uwekezaji au kujijengea usalama wa kifedha kwa sasa na siku zijazo. Ndiyo maana, kama taasisi ya kifedha, tunajiona kuwa mshirika wa safari hiyo ya maendeleo.

Akaunti ya NBC ni zaidi ya mahali pa kuhifadhi fedha; ni suluhisho kamili la kifedha mfano wa ‘wallet’ inayokuwezesha kufanya miamala ya kila siku kwa urahisi,ni mahali pa kuweka akiba, kutuma na kupokea pesa, kupata mikopo, kuwekeza katika masoko ya hisa na mifuko ya uwekezaji, pamoja na kuendesha biashara yako kwa ufanisi zaidi. Kupitia huduma hizi, tunalenga kukupa nyenzo na fursa zinazokusaidia kufikia malengo yako na kutimiza ndoto zako,” alisema.

Aliongeza kuwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja yana mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa taifa. Hivyo, kuwasaidia wananchi kupata elimu sahihi ya fedha, kuweka akiba, kuwekeza na kutumia huduma rasmi za mikopo ni njia muhimu ya kujenga uchumi jumuishi unaowanufaisha wengi zaidi.

“Kila tunapomsaidia mfanyabiashara kukuza mtaji wake, mkulima kuongeza uzalishaji, mzazi kuandaa mustakabali wa mtoto wake au kijana kuanza safari yake ya kifedha, tunakuwa pia tunachangia ukuaji wa uchumi wa nchi. Hiyo ndiyo maana halisi ya kuwaona Watanzania wakifika mbali,” alisisitiza.

Kupitia kampeni hiyo, NBC itatoa elimu ya kifedha na kuhamasisha matumizi ya bidhaa na huduma zake mbalimbali zilizobuniwa kulingana na mahitaji ya makundi tofauti ya kijamii. Miongoni mwa huduma hizo ni Akaunti ya Chanua kwa watoto, Akaunti ya Malengo, Akaunti ya Johari kwa wanawake, Akaunti ya Mwalimu, Akaunti ya Mshahara, Akaunti ya Wajasiriamali, Akaunti ya Waalimu, Akaunti ya Wanafunzi, Akaunti ya Kua Nasi, Akaunti ya Vikundi, Akaunti Binafsi, Akaunti ya Diaspora pamoja na Akaunti za Biashara pamoja na akaunti ya Muda Maalum kwa ajili ya uwekezaji.

Kwa upande wake, Meneja wa Bidhaa na Mauzo wa NBC, Bi. Dorothea Mabonye, alisema kampeni hiyo pia itatoa elimu kuhusu usimamizi wa fedha, matumizi sahihi ya mikopo, huduma za bima, mifumo ya malipo na miamala ya kidigitali ili kuwajengea wananchi uwezo wa kufanya maamuzi bora ya kifedha.

“Kupitia kampeni hii tunataka kuwasaidia Watanzania kutambua kuwa huduma za kifedha si kwa ajili ya kutunza fedha pekee, bali ni nyenzo muhimu ya kufikia malengo yao ya maisha. Tunataka kuona wananchi wakitumia huduma hizi kujenga msingi imara wa maendeleo yao na ya familia zao,” alisema.

Alifafanua kuwa huduma mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo zimebuniwa ili kukidhi mahitaji ya kila kundi. “Kwa mfano, wazazi wanaweza kuwawekea watoto wao msingi wa utamaduni wa kuweka akiba kupitia Akaunti ya Chanua huku wafanyakazi pia wakiweza kupata mkopo wa muda mfupi unaowasaidia kukidhi mahitaji ya dharura wanaposubiri muda wa kupokea mshahara’’ alisema

Aliongeza kuwa kupitia akaunti ya Diaspora Watanzania waishio nje ya nchi wanaweza kupata fursa rahisi za kuwekeza na kushiriki maendeleo ya nchi kupitia mikopo ya nyumba na akaunti ya muda maalum ya uwekezaji.

Naye Mkuu wa Huduma za Kidigitali wa NBC, Bw. Ulrik Peter, alisema teknolojia imeendelea kuwa daraja muhimu la kuwafikishia wananchi huduma za kifedha kwa haraka, kwa gharama nafuu na bila vikwazo vya umbali.

Alisema NBC imeendelea kuwekeza katika mifumo ya kidigitali kama vile NBC Kiganjani, NBC Connect, huduma za kadi za benki na mawakala ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma za kifedha bila kulazimika kutembelea matawi ya benki.

“Ujumuishaji wa kifedha hauwezi kufikiwa bila matumizi makubwa ya teknolojia. Kupitia kampeni hii tunawahamasisha wananchi kutumia huduma za kidigitali ambazo zinawawezesha kuokoa muda, kupunguza gharama za miamala na kupata huduma za kifedha popote walipo, wakati wowote na kwa namna wanayohitaji kufanya matumizi yao ya kila siku,” alisema.

Aliongeza kuwa uwekezaji uliofanywa na NBC katika mifumo ya kidigitali na utoaji wa kadi papo hapo kwa wateja wanaofungua akaunti mpya ni sehemu ya mkakati wa kuondoa vikwazo vinavyoweza kuwazuia wananchi kushiriki kikamilifu katika uchumi rasmi na kukua kiuchumi.



Maofisa mbalimbali wa Benki ya NBC wakiongozwa na Mkuu wa Bidhaa na Mauzo, Bw. Abel Kaseko (kushoto) wakipeperusha bendera kuashiria uzinduzi wa kampeni maalum inayofahamika kama “Tunakuona Mbali”, ikiwa ni sehemu ya jitihada za benki hiyo kuwawezesha Watanzania kutoka makundi mbalimbali ya kijamii kufikia malengo yao ya maendeleo kupitia huduma rasmi za kifedha. Hafla ya uzinduzi wa kampeni hiyo imefanyika leo jijini Dar es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...