Na Mwandishi Wetu

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Asangye Bangu, ameshiriki Jukwaa la Tanzania na Misri la Utalii, Biashara na Uwekezaji na kueleza kuwa Tanzania imeongeza biashara ya mifugo na mazao ya mifugo katika Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwa kuwa unazingatia uwazi, ubora na uaminifu katika biashara.

Akizungumza katika jukwaa hilo (Tanzania–Egypt Tourism, Trade and Investment Forum) lililofanyika nchini Misri na kuwakutanisha wadau wa biashara, uwekezaji na utalii, Bangu amesema mfumo unaotumika kusimamia biashara ya mazao ya kilimo sasa uko tayari kuhudumia pia sekta ya mifugo.

Akifafanua ufanisi wa matumizi ya mfumo huo katika moja ya mijadala iliyokuwepo kwenye jukwaa hilo, Bangu amesema wamefanya kikao kifupi na ujumbe wa Misri ambao wameonesha nia kubwa ya kufanya biashara ya mifugo na bidhaa zitokanazo na mifugo kutoka Tanzania.

“Tunawakaribisha wafanyabiashara wa Misri kuja kufanya biashara Tanzania. Mfumo wetu wa Stakabadhi za Ghala ni wa kuaminika na umejengwa kuhakikisha biashara inafanyika kwa uwazi na usalama kwa pande zote,” amesema.

Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Misri katika biashara ya mifugo na mazao mengine unaweza kuongeza thamani ya biashara kati ya nchi hizo mbili na kuwanufaisha wazalishaji, wafanyabiashara na uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Awali, amefafanua kuwa WRRB haihusiki na hatua ya uzalishaji wa mazao bali huingia baada ya uzalishaji kukamilika kwa kusimamia mnyororo wa biashara unaohakikisha bidhaa zinahifadhiwa, zinakaguliwa na kuuzwa kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa.

Bangu amesema kwa sasa WRRB inashirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), vyama vya ushirika pamoja na wafanyabiashara binafsi katika kuwezesha biashara ya mazao kupitia maghala yaliyosajiliwa na kusimamiwa kisheria.

Ameeleza kuwa bidhaa zinazopelekwa kwenye maghala hayo hukaguliwa ubora na kiasi chake na wataalamu mbalimbali kabla ya kuingizwa katika mfumo rasmi wa biashara.

“Maghala haya yanamilikiwa na sekta binafsi, vyama vya ushirika au Serikali, lakini yote husajiliwa na kusimamiwa na WRRB ili kuhakikisha yanazingatia viwango vinavyotakiwa,” amesema.

Kwa mujibu wa Bangu, mfumo huo unahusisha wataalamu wa ukaguzi wa ubora, usimamizi wa taarifa na ufuatiliaji wa bidhaa kuanzia zilikotoka hadi zinapowekwa ghalani, jambo linaloongeza uaminifu kwa wanunuzi wa ndani na nje ya nchi.

Ameongeza kuwa hatua ya mwisho ni kuandaliwa kwa taarifa kamili za bidhaa husika (catalogue) ambazo huwapatia wafanyabiashara taarifa muhimu kabla ya kufanya maamuzi ya ununuzi.

Bangu amesema WRRB pia inashirikiana na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) kupitia mfumo wa kidijitali unaowezesha wafanyabiashara kutoka sehemu mbalimbali duniani kuona bidhaa zilizopo maghalani na kufanya biashara kwa urahisi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...