Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kitaendelea kuunga mkono juhudi za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, za kuharakisha maendeleo ya wananchi huku kikisisitiza kuwa amani, umoja na mshikamano ni msingi muhimu wa maendeleo ya taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, alisema chama hicho kimeridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayofanywa na serikali katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, maji, umeme, barabara, kilimo na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.

Alisema katika ziara za chama zilizofanyika katika mikoa 12 na wilaya 41, viongozi wa CCM wamejionea mafanikio makubwa yaliyopatikana pamoja na kusikiliza changamoto za wananchi ili kuzitafutia ufumbuzi kupitia serikali.

“Tumeshuhudia kazi kubwa inayofanywa na serikali ya CCM chini ya Rais Samia. Fedha nyingi zimepelekwa katika miradi ya maendeleo na wananchi wanaendelea kunufaika na maboresho ya huduma za kijamii katika maeneo mbalimbali nchini,” alisema.

Kihongosi alisema pamoja na mafanikio hayo, baadhi ya changamoto zilizobainika ni migogoro ya ardhi, huduma ya maji katika maeneo machache na vitongoji ambavyo bado havijafikiwa kikamilifu na huduma ya umeme, huku akieleza kuwa serikali inaendelea kuzitatua kupitia bajeti na miradi inayoendelea kutekelezwa.

Alisema maendeleo ya taifa hayawezi kupatikana kwa siku moja bali yanahitaji muda, mipango na uwekezaji endelevu, akibainisha kuwa Tanzania ya sasa imepiga hatua kubwa ikilinganishwa na ilivyokuwa miaka mitano au 10 iliyopita.

Aidha, alimpongeza Rais Samia kwa kuendelea kufungua fursa za kiuchumi kupitia diplomasia ya kimataifa, hatua ambayo imeongeza uwekezaji na ushirikiano wa maendeleo kwa manufaa ya taifa.

Kuhusu Bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/27 ya zaidi ya Sh trilioni 62, Kihongosi alisema bajeti hiyo itaongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuboresha huduma muhimu kwa wananchi, huku akisisitiza kuwa ni ushahidi wa dhamira ya serikali ya kuendelea kuwaletea maendeleo Watanzania.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...