Na Said Mwishehe,Michuzi TV
MSANII maarufu nchini katika muziki wa kizazi kipya a.k.a Bongo Fleva Rashidi Makwiro maarufu Chid Benz ametoa ya moyoni kwa kuishukuru Mamlaka ya Kudhihiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na wote waliomuwezesha kuachana na matumizi ya dawa za kulevya.
Chid Benz ametoa shukrani hizo Juni 12,2026 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa filamu iliyopewa jina Kifurushi ambayo ni maalum kuelezea madhara ya dawa za kulevya.
Pia ni filamu inayotoa elimu kwa madereva,makondakta na abiria kuwa makini kwa kutosafirisha vifurushi ambavyo hawajui ndani yake kuna nini.Ni filamu iliyoandaliwa na mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Bodi ya Filamu Tanzania pamoja na LATRA.
Katika uzinduzi wa filamu hiyo msanii Chid Benz ambaye ubora wake katika muziki umeeendelea kubaki katika viwango vya daraja la juu aliyepewa jukum la kutoa burudani kupitia vibao vyake kadhaa kikiwemo Dar es Salaam Stand up alitumia nafasi hiyo kutoa shukrani zake kwani kwa sasa ameachana kabisa na dawa za kulevya .
“Kamishina wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo nakushukuru sana.Uliamua kunisaidia kuniondoa kwenye matumizi ya dawa za kulevya.Nakushukuru kwasababu pia nikikupigia simu unapokea,meseji unajibu.”
Akiendelea kuzungumza Chidi Benzi amesema “natamani niwaambie ndugu zangu tuache dawa za kulevya lakini sidhani kama sasa hivi watu wanatumia maana nahisi dawa hizo hazipo mtaani.Kuna saa zingine naongea na ndugu zangu nauliza vipi mtaani freshi wanaambia sio freshi.
“Kwahiyo hiyo kazi ambayo imefanyika ya kukomesha dawa za kulevya imefanyika kwa ukubwa kwani zamani ilikuwa kwa mfano nikikaa kama hapa nikiuliza eh bwana vipi hapa naambiwa freshi pita nyuma lakini sasa nakwambia ah sio freshi Chidi.”
Ameongeza kwa upande yeye ameacha kabisa kutumia dawa za kulevya na sasa hivi hata bila kumwambia mtu kama anatumia mtu mwenyewe anamuwahi kumwambia ameacha.
“Hivyo nashukuru Serikali, nashukuru Mamlaka ,nakushukuru kila mtu nashukuru na
leo tuko pamoja na kuonyesha kwamba nina nguvu za kutosha ninaburudisha,”amesema na kusisitiza naye anaungana na Mamlaka kuwahimiza wamiliki wa mabasi,madereva,makondakta na wananchi kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika kutoa taarifa.
Aidha amesema filamu hiyo iliyozinduliwa itasaidia kuongeza uelewa wa jamii na kuimarisha mapambano dhidi ya usafirishaji wa dawa za kulevya nchini.


.jpeg)





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...