Na Byera Deus Bukoba

Walimu walioko kazini pamoja na vijana ambao hawakufanikiwa kuendelea na elimu ya juu wametakiwa kutumia fursa zinazotolewa na vyuo vya elimu ya ujuzi vinavyotoa mafunzo kwa njia ya masafa ili kujiendeleza na kupata maarifa mapya yatakayowasaidia kukabiliana na mtaala mpya wa elimu.

Wito huo umetolewa wakati wa mahafali ya nne ya wahitimu wa DC Polytechnic Education Institute College kilichopo Halmashauri ya Bukoba mkoani Kagera, ambapo jumla ya wanafunzi 908 walihitimu katika ngazi za shahada na astashahada katika fani mbalimbali zikiwemo ualimu, utawala, uongozi, mawasiliano, teknolojia na ufundi.

Akizungumza katika Kongamano la Wahitimu (Convocation) la chuo hicho, Mkurugenzi wa Huduma za Jamii kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Elieth Lulu Niwagila, alisema Tanzania kwa muda mrefu imekuwa ikitekeleza mfumo wa elimu uliolenga zaidi utoaji wa maarifa ya darasani, lakini kwa sasa serikali imefanya maboresho makubwa ya mtaala ili kuzalisha wahitimu wenye umahiri, ubunifu na uwezo wa kutatua changamoto mbalimbali za jamii.

Alisema wataalamu wa elimu wamejiridhisha na mabadiliko hayo ya mtaala na kwamba walimu walioko kazini wanapaswa kujiendeleza ili kuendana na mahitaji ya mfumo mpya wa elimu.

“Niseme kwamba sisi kama wataalamu wa masuala ya elimu tumevutiwa sana na mabadiliko haya. Dunia imebadilika sana na kinachohitajika sasa ni ujuzi. Serikali imeamua kutoa elimu ya ujuzi kwa miaka 10; baada ya hapo mtoto akiona hawezi kuendelea, anaweza kujiajiri, na anayeendelea hadi chuo kikuu anaweza kuendelea na fani hiyo ya ufundi,” alisema Dkt. Niwagila.

Kwa upande wake, Meneja wa DC Polytechnic Education Institute College, Jackson Kailanga, alisema chuo hicho kinaendelea kutoa elimu katika fani mbalimbali kwa kuzingatia maboresho ya mtaala wa elimu yanayotekelezwa kupitia Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 pamoja na maboresho yake ya mwaka 2023.

Alisema maboresho hayo yanaweka mkazo katika elimu inayozingatia stadi za kazi, vitendo na mahitaji ya dunia ya sasa.

Kailanga alisema chuo hicho kinatoa fursa kwa watu walioko kazini ambao hawakupata nafasi ya kuendelea na elimu ya juu kwa kuwajengea uwezo na kuwapatia maarifa yanayowawezesha kuendana na mahitaji ya elimu ya sasa.

Aliongeza kuwa walimu walioko mikoani huunganishwa katika vituo maalumu vya mafunzo ambapo hupatiwa wataalamu wa kuwafundisha hadi wanapohitimu masomo yao.

Aidha, alisema chuo hicho kinawakaribisha vijana waliomaliza darasa la saba hadi kidato cha nne kujiunga na mafunzo ya ufundi katika nyanja mbalimbali ikiwemo ufundi wa magari, umeme na taaluma nyingine za kiufundi. Alisema wataalamu kutoka vyuo vya ufundi stadi vya VETA hushiriki katika kuwajengea uwezo wanafunzi wanaojiunga na chuo hicho.

Alitoa wito kwa vijana kutokata tamaa kwani zipo fursa nyingi za kujiajiri kupitia ujuzi na ubunifu. Pia aliwataka walimu walioko kazini kuendelea kujifunza na kupokea maarifa mapya ili kukabiliana na mabadiliko yanayoendelea katika sekta ya elimu.

Naye Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) Kanda ya Ziwa, Godfrey Michael, alisema mhitimu bora ni yule anayeweza kutumia maarifa aliyoyapata kuijenga jamii yake na kuharakisha maendeleo.

Aliwataka wahitimu kutumia elimu waliyoipata kama nyenzo ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii, kuongeza ujuzi unaohitajika kwa sasa, kuepuka vitendo vya rushwa na udanganyifu, na kuchangia utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu nchini.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...