Na Janeth Raphael MichuziTv - Bungeni Dodoma
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amesema Serikali imeweka mkazo mkubwa katika malezi, makuzi na ustawi wa watoto kama msingi wa kujenga Taifa lenye maadili, mshikamano na maendeleo endelevu kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akiwasilisha bungeni hotuba ya mapitio ya utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya mwaka 2025/26 pamoja na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2026/27, Dkt. Gwajima alisema Wizara yake imejipanga kutekeleza vipaumbele saba vya kimkakati vitakavyochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa manufaa ya Watanzania wote.
Ameeleza kuwa katika mwaka wa fedha 2026/27, Wizara itajikita katika maeneo yenye uwezo mkubwa wa kuleta mageuzi ya kijamii na kiuchumi, huku ikilenga kujenga Tanzania yenye jamii imara, jumuishi na inayozingatia maendeleo endelevu.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, kipaumbele cha kwanza kitakuwa ni kujenga mtaji watu wa Taifa na kuandaa kizazi cha Tanzania ya mwaka 2050 kitakachozingatia maadili, uzalendo, haki, usawa, ustawi na maendeleo jumuishi. Alisema Serikali inaamini kuwa watu ndiyo rasilimali muhimu zaidi katika safari ya maendeleo ya Taifa.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali itaendelea kuimarisha huduma za ustawi, malezi na makuzi ya watoto pamoja na mifumo ya ulinzi wa kijamii ili kuhakikisha kunakuwa na Taifa lenye mshikamano, uthabiti na utu wa kibinadamu.
Katika eneo la usawa wa kijinsia, Dkt. Gwajima amesema Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya uwezeshaji wa wanawake na kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia ili kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na uchumi wa Taifa.
Pia ameeleza kuwa Wizara inalenga kufanya mageuzi ya kiuchumi kwa makundi maalum na sekta isiyo rasmi kwa kuwasaidia wananchi kutoka katika uchumi wa kujikimu na kuingia katika uchumi rasmi wa kibiashara wenye tija, ushindani na mchango mkubwa katika pato la Taifa.
Kwa upande wa matumizi ya teknolojia, Waziri huyo alisema Serikali itaongeza matumizi ya mifumo ya kidijitali na takwimu katika utoaji wa huduma za kijamii ili kurahisisha utendaji kazi na kuhakikisha maamuzi yanafanyika kwa kuzingatia ushahidi wa kitakwimu.
Ameongeza kuwa juhudi pia zitaelekezwa katika kujenga jamii yenye amani, uwajibikaji na mshikamano pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya Serikali, Asasi za Kiraia, sekta binafsi, taasisi za dini na wadau wa maendeleo.
Dkt. Gwajima amesema kupitia vipaumbele hivyo, Serikali inalenga kujenga jamii salama na yenye ustawi, wanawake wenye nguvu kiuchumi, watoto waliopata malezi bora, pamoja na uchumi jumuishi unaochochewa na maarifa, teknolojia na ubunifu.
Amesisitiza kuwa bajeti ya Wizara hiyo imeweka kipaumbele katika huduma za ustawi wa jamii, uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, huduma kwa watoto, wazee, wanawake, wanaume na makundi mengine maalum, akibainisha kuwa huduma hizo ni sehemu muhimu ya kulinda amani, usalama na uthabiti wa Taifa.
“Hatutapima mafanikio ya bajeti hii kwa kiasi cha fedha kilichotumika pekee, bali kwa matokeo yatakayopatikana kwa familia, wananchi na Taifa kwa ujumla,” alisema.
Katika sehemu ya hotuba yake iliyovuta hisia za wabunge, Waziri huyo aliweka msisitizo mkubwa kwenye suala la malezi ya watoto, akisema ndilo jambo linalobeba mustakabali wa Tanzania kuliko jambo jingine lolote.
Ameeleza kuwa pamoja na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika miundombinu mbalimbali ikiwemo reli za kisasa, bandari, viwanja vya ndege na miji ya kisasa, mafanikio hayo hayatakuwa na maana ikiwa Taifa litashindwa kujenga watoto wenye maadili, nidhamu, uzalendo, utu na uwezo wa kushindana katika dunia ya mwaka 2050.
“Taifa lolote hujengwa kwanza kwenye malezi kabla halijajengwa kwenye uchumi. Mtoto wa leo ndiye mtendaji wa Serikali wa kesho, daktari wa kesho, mwalimu wa kesho, jaji wa kesho, askari wa kesho, mwekezaji wa kesho na kiongozi wa Taifa wa kesho,” alisema.
Ameonya kuwa kuharibu malezi ya watoto wa leo ni sawa na kuharibu Tanzania ya kesho, akisisitiza umuhimu wa familia, jamii na taasisi mbalimbali kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha watoto wanalelewa katika misingi ya maadili mema, uzalendo na uwajibikaji.
Dkt. Gwajima alihitimisha kwa kueleza kuwa utekelezaji wa mpango na bajeti ya mwaka 2026/27 umeandaliwa mahsusi kuleta matokeo yanayopimika, kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma, kupunguza umaskini, kulinda makundi yaliyo hatarini na kuimarisha mshikamano wa Kitaifa kuelekea kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...