Na Janeth Raphael MichuziTv


Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) anayeshughulikia Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, amesema chama hicho kimepokea taarifa zinazoonyesha kuwepo kwa baadhi ya makundi yanayodaiwa kupanga njama za kuvuruga amani na utulivu wa nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo, Kihongosi amesema CCM imepata taarifa za kuaminika kwamba baadhi ya vyama vya upinzani vinafanya vikao vya siri vinavyolenga kuleta taharuki na kuvuruga hali ya amani iliyopo nchini.

Kutokana na hali hiyo, amewasihi Watanzania kuendelea kuwa walinzi wa amani na kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha usalama, mshikamano na utulivu wa taifa.

“Tunawaomba Watanzania wote kutoshiriki katika mipango au vitendo vyenye nia ya kuvuruga amani ya nchi. Amani ndiyo msingi wa maendeleo yetu, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuilinda na kuitunza,” amesema Kihongosi.

Aidha, amesisitiza kuwa vijana wana nafasi muhimu katika kulinda amani na utulivu wa nchi kutokana na wingi wao na ushawishi mkubwa waliounao katika jamii.

Kihongosi amesema kuna baadhi ya watu ambao wameamua kwenda kinyume na maslahi ya taifa kwa kujiunga na makundi yenye malengo ya kuvuruga amani, akiwataka wananchi kutokubali kushawishiwa na makundi hayo.

Pia amewataka vijana kuwa makini na macho dhidi ya watu au vikundi vinavyoweza kuwatumia kama nyenzo za kutekeleza agenda zinazoweza kuhatarisha usalama wa nchi.

Wakati huo huo, Kihongosi amewataka wananchi kuendelea kumuunga mkono Samia Suluhu Hassan katika juhudi zake za kuimarisha amani, umoja na utulivu wa taifa.

“Amani na utulivu ni nguzo muhimu ya maendeleo ya nchi yetu. Ni jukumu la kila Mtanzania kuhakikisha tunailinda kwa nguvu zote kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” amesisitiza.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...