Na Said Mwishehe,Michuzi TV

SIKU za karibuni Chama Cha Mapinduzi(CCM) kupitia Katibu Mkuu wake Dk.Asha-Rose Migiro kimevunja ukimya wa muda mrefu kwa kuamua kuzungumzia masuala mbalimbali tangu kutokea kwa vurugu Oktoba 29.

Kupitia mahojiano maalum yaliyofanywa na Mtangazaji wa Crown Media Salim Kikeke alitumia nafasi hiyo kuuliza maswali mbalimbali kwa CCM kupitia Katibu Mkuu Dk.Asha-Rose Migiro.

Kwa sehemu kubwa maswali ya Kikeke yalijikita katika ripoti ya Tume ya Kuchunguza matukio kabla na baada ya Oktoba 29 mwaka 2025.Tume hiyo ilikuwa ikiongozwa na Mwenyekiti Jaji Mstaafu Othman Chande.

Tunafahamu tangu kutolewa kwa ripoti hiyo ambayo ilikabidhiwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan kumekuwepo na maswali mengi na kwa CCM tangu kutolewa kwa ripoti hiyo ilikuwa kimya.

Kwa majibu ya Katibu Mkuu wa CCM, Asha-Rose Migiro, inaonesha jambo moja muhimu ambalo viongozi wa chama hicho wameamua kulifanya baada ya kutolewa kwa ripoti ya Tume iliyoongozwa na Othman Chande; kwanza ni kutafakari kwa kina kabla ya kutoa msimamo rasmi wa kisiasa.

Kwa muda mrefu baada ya ripoti hiyo kutolewa, kulikuwa na maswali mengi kutoka kwa wananchi kuhusu ukimya wa CCM. Hata hivyo, katika majibu yake, Dk. Migiro ameonesha kuwa chama hakikutaka kutoa majibu ya haraka kutokana na uzito wa tukio lenyewe. 

Kauli yake kwamba viongozi wa CCM “waliduwaa” na “walishutuka” inaashiria kuwa chama kiliona matukio ya Oktoba 29 kama jambo lisilo la kawaida katika historia ya Tanzania. 

Hivyo, badala ya kujibu kwa haraka au kwa hisia, walichagua kuchukua muda wa kutafakari kilichotokea na athari zake kwa taifa.

Mtazamo huo unaonesha CCM imepokea ripoti ya Jaji Chande si kama nyaraka za kawaida za kisiasa, bali kama taarifa inayohitaji tathmini ya kina ya kitaifa. 

Ndiyo maana Migiro amesisitiza mara kadhaa kuwa ripoti hiyo imepokelewa kwa umakini mkubwa na kwamba chama kinataka kufahamu kwa undani nini kilitokea ili matukio hayo yasijirudie tena katika historia ya nchi.

Jambo jingine linalojitokeza ni kwamba CCM imeamua kuipa hadhi na heshima kubwa Tume ya Jaji Chande. Katika majibu yake, Dk.Migiro hajajaribu kubishana na takwimu zilizotolewa wala kuhoji uhalali wa kazi iliyofanywa na tume hiyo. 

Badala yake, amepongeza kazi ya tume, amewapongeza wananchi walioshiriki kutoa ushahidi na hata kusisitiza kuwa chama hakina sababu ya kutilia shaka vyanzo vya taarifa vilivyotumiwa kufikia hitimisho la ripoti hiyo. 

Binafsi niliamua kuifuatilia mahoajiano yake,nikawa makini kusikiliza maswali ya Kikeke lakini ukweli nilituliza akili yangu zaidi kusikiliza majibu ya Dk.Migiro ,mwanamama mbobebu katika siasa za kitaita na kimataifa.

Kupitia majibu ya Dk.Migiro nilibaini CCM imeamua kuikubali ripoti hiyo kama nyenzo muhimu ya kuelewa kilichotokea na kutafuta suluhisho la kudumu.

Aidha, majibu yake yanaonesha CCM imechagua kutenganisha masuala mawili makubwa yaliyokuwa yakijadiliwa na wananchi. Kwanza ni suala la kusikitishwa na vifo vya watu 518 vilivyotajwa katika ripoti. 

Pili ni suala la kutambua mchango wa vyombo vya ulinzi na usalama katika kuzuia hali isizidi kuwa mbaya zaidi. Migiro anajenga hoja kwamba inawezekana kukawa na makosa yaliyofanyika katika utekelezaji wa majukumu, lakini hilo haliondoi umuhimu wa kutambua jukumu la msingi lililofanywa na vyombo hivyo katika kulinda usalama na utulivu wa nchi wakati wa tukio hilo.

Katika eneo hilo ndipo unaonekana mkakati wa kisiasa wa CCM. Chama hakijakubali hoja kwamba pongezi zilizotolewa kwa vyombo vya ulinzi na usalama zilikuwa ni kufumbia macho madhara yaliyotokea. 

Badala yake, kinaeleza kuwa pongezi hizo zilihusu jukumu la jumla la kulinda utulivu wa taifa wakati uchunguzi wa kina kuhusu vifo na madhara mengine ukiendelea kufanyika kupitia mifumo ya kisheria.

Pia kuna ujumbe muhimu wa kisiasa ambao CCM inaonekana kuutuma kupitia Katibu Mkuu wake. Chama kinataka kuondoa taswira kwamba vyombo vya dola vinafanya kazi kwa ajili ya kukilinda CCM badala ya kulinda taifa. 

Katika majibu yake, Migiro anasisitiza kuwa kabla ya Oktoba 29 kampeni na shughuli za uchaguzi zilifanyika kwa utulivu nchini kote bila hitaji kubwa la kuingilia kati kwa vyombo vya usalama. 

Kwa mtazamo wa CCM, tukio la Oktoba 29 linaonekana kutazamwa zaidi kama changamoto ya kiusalama kuliko tukio la ushindani wa kisiasa.

Hata hivyo, swali gumu zaidi ambalo Migiro alikabiliana nalo ni kuhusu uwajibikaji. Hili ndilo eneo ambalo wananchi wengi wamekuwa wakisubiri kuona hatua za moja kwa moja baada ya ripoti ya Jaji Chande kutaja vifo na madhara mengine yaliyotokea. 

Badala ya kutaja watu binafsi wanaopaswa kuwajibika mara moja, Dk.Migiro amehamishia matumaini ya CCM kwenye tume ya uchunguzi wa jinai iliyoundwa kufuatilia kwa kina matukio hayo. 

Kauli hiyo inaonesha kuwa chama kinaamini uwajibikaji lazima ujengwe juu ya ushahidi wa kisheria na matokeo ya uchunguzi rasmi, badala ya maamuzi yanayotokana na shinikizo la kisiasa au hisia za wakati huo.

Kwa ujumla, majibu ya Dk. Migiro yanaonesha CCM imepokea ripoti ya Jaji Chande kwa njia tatu kuu. Kwanza, kama nyaraka muhimu ya kujifunza kilichotokea. Pili, kama msingi wa kutafuta namna ya kuzuia matukio kama hayo yasijirudie tena siku zijazo. 

Tatu, kama mwanzo wa mchakato wa uwajibikaji ambao chama kinaamini unapaswa kuongozwa na sheria, ushahidi na taasisi husika za uchunguzi.

Kwa mtazamo mpana zaidi, mahojiano hayo yanaashiria CCM imeamua kusimama katikati ya hoja mbili zinazovutana; upande mmoja kutetea uthabiti wa taasisi za dola na upande mwingine kukubali kuwa kuna maswali mazito yanayohitaji majibu kuhusu vifo na madhara yaliyotokea Oktoba 29. 

Huo ndio mwelekeo unaojitokeza katika namna viongozi wa chama walivyopokea, kutafakari na kuanza kuijadili hadharani ripoti ya Jaji Chande baada ya kipindi kirefu cha tathmini ya ndani ya chama.

Nihitimishe kwa kumpongeza Katibu Mkuu Dk.Asha-Rose Migiro kwa utulivu wake alipokuwa akijibu maswali ya Salim Kikeke,pili nampongeza Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayofanya katika kukisimamia na kukiongoza Chama hicho kwa utulivu mkubwa.

Pamoja na hayo nitoe rai kwa Watanzania wote kwa umoja wetu tunapaswa kutambua tunayo nafasi ya kuhakikisha tunailinda nchi yetu kwa wivu mkubwa.Umoja na mshikamano ndio silaha yetu.

Tumshukuru Mungu kwa kuendelea kutuweka katika mikono yake na hatimaye licha ya yale yaliyotokea Oktoba 29 kama

Taifa tumeendelea kuwa wamoja na shughuli zetu za uzalishaji zinaendelea.Kwa pamoja tuseme ahsante Mwenyezi Mungu muumba wa mbingu na aridhi na vyote vilivyomo.


Ukipiga tu nipomepokea kwani 

shida iko wapi mtu wangu

Simu 0713833822/0762451570

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...