Na Janeth Raphael MichuziTv
Sekta ya Maliasili na Utalii imetajwa kuwa miongoni mwa sekta muhimu zinazochangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya taifa kupitia ukuaji wa uchumi, upatikanaji wa ajira, mapato ya serikali na ustawi wa jamii zinazoishi pembezoni mwa maeneo ya hifadhi.
Hata hivyo, mafanikio ya sekta hiyo yameendelea kuambatana na changamoto ya kuhakikisha kuwa uhifadhi wa wanyamapori unaendana na ulinzi wa maisha, mali na shughuli za kiuchumi za wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya hifadhi. Kutokana na hali hiyo, Serikali imeendelea kuweka kipaumbele katika kutafuta suluhisho endelevu la migongano kati ya binadamu na wanyamapori wakali na waharibifu.
Akizungumza leo jijini Dodoma wakati akimwakilisha Waziri wa Maliasili na Utalii kufunga Mkutano wa Mwaka wa Wahifadhi wa Wanyamapori nchini, Mkurugenzi wa Wanyamapori Tanzania, Dkt. Alexander Lobora, amesema Serikali imeimarisha mifumo ya usimamizi wa migogoro hiyo kupitia sera mbalimbali, mikakati pamoja na matumizi ya teknolojia ya kisasa.
Amesema mfumo huo mpya unalenga kuongeza uwazi na uwajibikaji katika mchakato wa kushughulikia madai ya fidia ya “kifuta jasho na machozi” kwa wananchi wanaoathirika na wanyamapori.
Dkt. Lobora amesisitiza kuwa kuanzia tarehe 1 Julai 2026, Wizara haitapokea tena madai ya fidia kwa njia ya karatasi, bali yote yatapokelewa kupitia mfumo wa kidigitali ulioboreshwa. Ameelekeza maafisa wote kuhakikisha wanatumia mfumo huo kikamilifu katika maeneo yao ya kazi, kuingiza taarifa kwa usahihi na kuwasilisha kwa wakati.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya mfumo huo, kuhakikisha taarifa zote zinakuwa sahihi, pamoja na kuhakikisha mawasiliano ya waombaji yanathibitishwa ipasavyo kupitia namba za simu zinazotambulika. Pia amekumbusha watumishi wa umma kuzingatia maadili na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Wanyamapori, Dkt. Fortunata Msoffe, amesema ongezeko la shughuli za kibinadamu kuelekea maeneo ya hifadhi na kwenye shoroba za wanyamapori limechangia kuongezeka kwa matukio ya migogoro hiyo na kusababisha madhara kwa jamii.
Ameeleza kuwa Wizara imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kupunguza changamoto hizo, ikiwemo kufanya doria za mara kwa mara, kuongeza kasi ya mwitikio wa matukio, kutoa elimu kwa wananchi na kuimarisha usimamizi wa maeneo ya hifadhi pamoja na shoroba za wanyamapori kwa kutumia teknolojia za kisasa kufuatilia mienendo ya wanyama.
Kwa upande wa Serikali za Mitaa, Afisa Misitu Mkuu kutoka TAMISEMI, Rogasian Philip, ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuendelea kutekeleza sera ya ugatuaji wa madaraka, akisema hatua hiyo imeongeza ufanisi katika usimamizi wa rasilimali za misitu na wanyamapori.
Naye Afisa Kilimo wa Kata ya Kiambai, Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Anna Roki, amesema mfumo huo mpya utarahisisha utendaji kazi ikilinganishwa na mfumo wa awali wa kutumia fomu za karatasi, ambao ulikuwa unachukua muda na kuongeza ugumu wa huduma kwa wananchi.
Ameongeza kuwa mfumo wa kidigitali utasaidia wananchi kupata stahiki zao kwa haraka zaidi na kupunguza malalamiko yaliyokuwa yakijitokeza hapo awali.
Serikali imesisitiza kuwa matumizi ya teknolojia katika usimamizi wa migogoro ya binadamu na wanyamapori ni hatua muhimu kuelekea ufanisi zaidi, uwazi na uboreshaji wa huduma kwa wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya hifadhi.









Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...