Na Janeth Raphael MichuziTv
📌Mlima Mautia waendelea kuibua msisimko wa kisayansi kutokana na Yoderite adimu
Katika safari ya dunia kugundua maajabu ya asili na historia ya mabadiliko ya sayari, Tanzania imeendelea kujitokeza kama moja ya mataifa yenye hazina adimu za kijiolojia. Mojawapo ya maeneo yanayozidi kuvutia macho ya watafiti na watalii wa kisayansi ni Mlima Mautia uliopo wilayani Kongwa, mkoani Dodoma, unaotajwa kuwa na historia ya kipekee duniani kutokana na uwepo wa madini adimu ya Yoderite.
Kwa mujibu wa wataalamu wa jiolojia kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), mlima huo ni miongoni mwa maeneo yenye thamani kubwa ya kisayansi, si tu Tanzania bali pia katika ramani ya jiolojia ya dunia, kutokana na mabadiliko makubwa ya kijiolojia yaliyotokea na kuzaa madini hayo adimu.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara ya kitaalamu iliyofanyika leo Juni 30, 2026, Meneja wa Idara ya Jiolojia wa GST, Maswi Solomoni, amesema Mlima Mautia unatoa ushahidi hai wa historia ya mabadiliko ya tabaka la dunia kupitia miamba na madini yaliyomo ndani yake.
Amefafanua kuwa madini ya Yoderite yaligunduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1959 na mtaalamu wa jiolojia kutoka Marekani, Hatten Yoder, ambaye baadaye jina lake lilitumika kuyatambulisha madini hayo kama heshima kwa mchango wake mkubwa katika tafiti za kisayansi.
“Baada ya kugunduliwa Tanzania mwaka 1959, madini haya yaliaminika kuwa ya kipekee duniani kwa muda mrefu, hadi mwaka 1998 yalipogunduliwa tena katika ukanda wa Zambezi nchini Zimbabwe,” alisema Solomoni.
Kwa mujibu wake, ugunduzi huo wa awali umeifanya Tanzania kutambulika kimataifa kama sehemu ya mwanzo kabisa ambapo madini ya Yoderite yalipatikana, jambo linaloongeza hadhi ya taifa katika ramani ya utafiti wa jiolojia duniani.
Solomoni alisisitiza kuwa Mlima Mautia una uwezo mkubwa wa kuwa kituo muhimu cha utalii wa jiolojia (geotourism), ambapo watafiti, wanafunzi wa sayansi ya ardhi, wanajiolojia pamoja na watalii kutoka sehemu mbalimbali duniani wanaweza kuutembelea kujifunza historia ya malezi ya dunia kupitia miamba yake ya kipekee.
Amebainisha kuwa muundo na historia ya kijiolojia ya mlima huo haujafananishwa na maeneo mengi duniani, jambo linaloufanya kuwa kama “maabara ya asili” kwa tafiti za kisayansi na elimu ya jiolojia.
Wataalamu wanaamini kuwa iwapo kutakuwa na uwekezaji wa kutosha katika uhifadhi, utafiti na utangazaji wa Mlima Mautia, Tanzania inaweza kujijengea nafasi kubwa kama moja ya vituo vinavyoongoza barani Afrika katika utalii wa jiolojia, huku sekta hiyo ikichangia zaidi katika kukuza uchumi wa taifa kupitia utalii wa kisayansi.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...