Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amekutana na mwanazuoni na mhamasishaji wa dhana ya Utalii Halali Duniani, Bw. Ismail Bullock kutoka Dubai.

Mazungumzo hayo yamefanyika leo, tarehe 03 Juni 2026, Ikulu Zanzibar, alipofika kujitambulisha pamoja na ujumbe alioambatana nao kutoka Taasisi ya Samia Foundation.

Rais Dkt. Mwinyi amesifu kazi nzuri anayofanya mwanazuoni huyo katika kutangaza na kuhamasisha Utalii Halali katika mataifa mbalimbali duniani, na kuahidi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaridhishwa na inaunga mkono juhudi zake za kukuza na kuendeleza utalii unaofuata misingi ya Kiislamu.

Aidha, amesema Zanzibar itaendelea kujifunza zaidi kupitia uhamasishaji na mafunzo anayoyatoka kwa wadau wa sekta ya utalii, na kumshauri kuendelea na jukumu hilo kutokana na manufaa makubwa yanayopatikana kwa nchi na wadau wa utalii katika kufahamu njia bora na sahihi za kutekeleza Utalii Halali (Halal Tourism).

Dkt. Mwinyi amepongeza hatua ya Bw. Ismail Bullock ya kuchapisha na kusambaza nakala za Kitabu Kitakatifu cha Qur'an kilichotafsiriwa kwa lugha ya Kiingereza, akieleza kuwa ni hatua muhimu inayoweza kuwasaidia wadau wengi zaidi kuelewa dhana ya Utalii Halali, na kumhakikishia ushirikiano zaidi.

Naye mwanazuoni Bw. Ismail Bullock amesema dhamira yake kuu ni kuona dhana ya Utalii Halali inaeleweka na kutekelezwa katika mataifa mbalimbali duniani. Amesema tayari dhana hiyo imeendelea kupata umaarufu mkubwa katika nchi nyingi duniani.

Bw. Ismail Bullock kwa sasa, yupo Zanzibar ambako anaendelea kutoa mafunzo kwa wadau wa sekta ya utalii kuhusu dhana ya Utalii Halali.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...