Na Said Mwishehe,Michuzi TV

RAIS wa Singapore Tharman Shanmugaratnam amesema kwamba maendeleo ya ujuzi, upanuzi wa nishati, taasisi imara na ujumuishaji wa kifedha kuwa maeneo muhimu ambayo Tanzania inapaswa kuyaimarisha ili kutekeleza kwa mafanikio Dira ya Taifa ya 2050.

Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza katika mhadhara wa wazi uliofanyika jana katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wenye mada “Kuwekeza katika Vichocheo vya Ukuaji Jumuishi”,

Mhadhara huo wa wazi umeandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushiriano wa Afrika Mashariki,Taasisi ya Uongozi pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) ambapo Rais Tharman ametumia nafasi hiyo kueleza kwamba Tanzania ina misingi imara ya ukuaji wa baadaye, ikiwemo idadi kubwa ya vijana, rasilimali nyingi za asili na utulivu wa kisiasa.

Amefafanua kuwa kugeuza faida hizo kuwa ustawi endelevu kutahitaji uwekezaji wa makusudi katika rasilimali watu, miundombinu na taasisi zenye ufanisi huku elimu na maendeleo ya ujuzi vinapaswa kubaki kuwa kiini cha ajenda ya maendeleo ya Tanzania, akieleza kuwa nchi zitakazofanikiwa katika siku zijazo ni zile zinazowekeza daima kwa watu wake.

“Mifumo ya elimu lazima iwaandae vijana kwa soko la ajira ambalo linaendelea kubadilishwa na maendeleo ya teknolojia, otomatiki (automation) na akili mnemba (Artificial Intelligence), huku pia ikitoa fursa kwa wafanyakazi kuendelea kuboresha ujuzi wao katika maisha yao ya kazi.”

Pia ameitaja nishati ya uhakika na yenye gharama nafuu kuwa kichocheo muhimu cha mabadiliko ya kiuchumi na kusisitiza uendelezaji wa viwanda, matumizi ya teknolojia za kidijitali na uundaji wa ajira vinategemea upatikanaji wa nishati ya kutosha, hivyo kufanya uwekezaji katika uzalishaji na usambazaji wa umeme kuwa muhimu kwa ukuaji wa muda mrefu.

“Taasisi imara na utawala bora pia ni muhimu katika kufikia maendeleo endelevu.Pia uthabiti wa sera, uwazi na imani ya wananchi husaidia kujenga mazingira yanayovutia uwekezaji, kuhimiza ubunifu na kuhakikisha manufaa ya ukuaji wa uchumi yanawanufaisha wananchi wengi,”amesema.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa ujumuishaji wa kifedha kama sehemu muhimu ya maendeleo ya kiuchumi, akibainisha kuwa upatikanaji mpana wa huduma za kifedha unaweza kuziwezesha kaya, kusaidia ujasiriamali na kupanua fursa za kiuchumi.

Pia ameeleza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi, akisema mikakati yenye mafanikio ya maendeleo inahitaji ushirikiano unaoweza kuhamasisha mtaji, teknolojia na utaalamu.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo, amesema mhadhara huo umeakisi ushirikiano unaozidi kuimarika kati ya Tanzania na Singapore wakati nchi hizo mbili zikiadhimisha miaka 45 ya uhusiano wa kidiplomasia.

“Tanzania inathamini uzoefu wa Singapore katika maendeleo na inaona fursa kubwa za kuimarisha ushirikiano katika biashara, uwekezaji, utawala wa umma, maendeleo ya ujuzi na mageuzi ya kiuchumi.”

Awali Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye, amesema taasisi hiyo imeheshimiwa kuwa mwenyeji wa mhadhara huo, akiueleza kuwa ni jukwaa muhimu la kubadilishana mawazo kuhusu ukuaji jumuishi na maendeleo ya taifa.

“Mawazo na uzoefu wa Rais Tharman utachangia mijadala inayoendelea kuhusu matarajio ya maendeleo ya muda mrefu ya Tanzania na utekelezaji wa Dira ya 2050.”

Mhadhara huo wa wazi ulikuwa sehemu ya ziara ya kiserikali ya siku tatu ya Tharman nchini Tanzania.














Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...