-Lumbila Wapata Umeme kwa Mara ya Kwanza Tangu Uhuru

-Giza la Miaka 60 Lamalizika Wilayani Ludewa


Ludewa, Njombe📍

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na mkandarasi; Shirika la Uzalishaji Mali JKT (SUMA JKT) leo, tarehe 25 Juni, 2026 kwa mara ya kwanza wamewasha umeme katika kitongoji cha Lumbila katika Halmashauri ya wilaya ya Ludewa ambapo eneo hilo lilikuwa halijapa umeme tangu Tanzania ipate uhuru wake 9 Desemba, mwaka 1961.

Akiongoza hafla hiyo ya kuwasha umeme kwa mara ya kwanza, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB); Bodi inayoisimamia REA; Mhe. Balozi na Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu alisema utekelezaji wa mradi huo ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia Watanzania wote bila kujali umbali na changamoto za kijiografia.

Eneo hili lilikuwa halijawahi kupata umeme kwa zaidi ya miaka 60 tangu Tanzania ipate uhuru wake mwaka 1961. Hafla hiyo ya kuwasha umeme kwa mara ya kwanza katika Kitongoji cha Lumbila imefanyika katika Kanisa Katoliki la Kitongoji cha Lumbila, hatua iliyopokelewa kwa furaha kubwa na Wananchi wa eneo hilo.

Awali kabla ya kumkaribisha Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB); Mheshimiwa Balozi na Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu, Mhandisi, Thomas Mmbaga amaye alimwakilisha Mkurugenzi wa Umeme Vijijini alisema, Mradi wa kusambaza umeme kwenye vitongoji sita vya mwambao wa Ziwa Nyasa umetumia gharama ya Shilingi bilioni 3.124 na kuongeza kuwa hadi sasa mradi umefikia asilimia 67, ambapo vitongoji 3 kati ya 6 vya mwambao wa Ziwa Nyasa vimeshawashiwa umeme.

Mhandisi Mmbaga ameongeza kuwa Mradi unahusisha ujenzi wa kilomita 36.6 za njia za msongo wa kati na kilomita 15.1 za msongo mdogo.

“Mradi unatarajiwa kuwafikia wateja 151 wa njia moja (single-phase) na wateja 9 wa njia tatu (three-phase). Tayari kaya zaidi ya 23 zimeomba kuunganishiwa”. Amekaririwa, Mhandisi, Mmbaga.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya SUMA JKT Company Ltd, Meja James Simon Mwame, alisema utekelezaji wa Mradi huo ulikuwa na changamoto kubwa kutokana na mazingira ya mwambao wa Ziwa Nyasa, lakini juhudi za wataalam na wafanyakazi wa kampuni hiyo zimewezesha ndoto ya Wananchi kupata umeme kutimia.

Meja Mwame alisema SUMA JKT ni kampuni inayojihusisha na ujenzi na usambazaji wa miundombinu ya umeme nchini, na kwa Mkoa wa Njombe kampuni hiyo inatekeleza miradi ya usambazaji umeme katika wilaya za Ludewa na Makete.

Ziara ya viongozi (ikiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Balozi Jacob Kingu) ilihusisha safari ya majini kwa boti ya takribani kilomita 11 kutoka Pwani ya Matema (Kyela, Mbeya) hadi Ludewa kutokana na ugumu wa kijiografia na miundombinu ya usafirishaji wa vifaa.

Mwananchi wa eneo hilo, Bakari Gowele, amebainisha kuwa umeme huo utasaidia sana sekta ya uvuvi kwani sasa wataweza kutengeneza barafu na kuhifadhi samaki kwa muda mrefu ili kuwafikisha kwenye masoko ya mbali wakiwa katika ubora wa hali ya juu.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...