SERIKALI YAFAFANUA JINSI WANAWAKE WA VIJIJINI WANAVYONUFAIKA NA MIKOPO YA ASILIMIA 10 YA HALMASHAURI


Na Janeth Raphael MichuziTv Bungeni - Dodoma 


Serikali imeeleza kuwa imeweka mifumo na taratibu mbalimbali za kuhakikisha wanawake wa vijijini wanapata fursa sawa ya kunufaika na mikopo inayotolewa kupitia asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri nchini.

Kauli hiyo imetolewa bungeni na Naibu  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Dkt Festo Ndugange wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Dkt. Neema Peter Majule, aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kuhakikisha fedha hizo zinawafikia wanawake wa vijijini.

DKt Ndugange amesema kuwa kwa sasa utoaji wa mikopo hiyo unafanyika kupitia mfumo wa kielektroniki wa WEZESHA Portal, ambao umeboreshwa ili kutoa nafasi kwa makundi maalumu, ikiwemo wanawake wa vijijini, kuwasilisha maombi yao kwa urahisi na kwa wakati.

Amesema pamoja na matumizi ya mfumo huo wa kidijitali, Serikali imewaelekeza Watendaji wa Kata na Vijiji kuwasaidia wananchi wa maeneo ya vijijini, hususan wanawake, katika mchakato wa usajili na uwasilishaji wa maombi ya mikopo ili kuondoa changamoto kwa wale wasiokuwa na uelewa wa kutosha wa TEHAMA au vifaa vya mawasiliano.

“Lengo ni kuhakikisha hakuna mwanamke anayekosa fursa ya kupata mkopo kutokana na changamoto za matumizi ya teknolojia. Watendaji wa Serikali katika ngazi za chini wamepewa jukumu la kuwawezesha wanawake wa vijijini kufikia huduma hii kwa urahisi,” alisema Waziri huyo.

Aidha, Serikali imeeleza kuwa imeimarisha mfumo wa uhakiki wa waombaji ili kuhakikisha walengwa halisi ndio wanaonufaika na mikopo hiyo. Uhakiki huo unafanyika kuanzia ngazi ya Kamati za Maendeleo ya Kata (WDC), ambazo hupitia maombi yote kabla ya kuidhinishwa.

Hatua hiyo inalenga kuzuia vikundi visivyostahili kutumia anwani za vijijini kwa lengo la kupata mikopo pamoja na kuhakikisha fedha zinawafikia wananchi wa maeneo yaliyokusudiwa.

Kwa upande wa utekelezaji, Serikali imesema mwenendo wa utoaji wa mikopo kwa wanawake umeendelea kuimarika na kuzidi matarajio yaliyowekwa. Takwimu zinaonesha kuwa katika kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2026, Serikali ilipanga kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 112.29 kwa wanawake, lakini hadi kufikia Machi 2026 jumla ya shilingi bilioni 136.01 zilikuwa zimetolewa.

Kiasi hicho ni sawa na utekelezaji wa asilimia 121 ya lengo lililowekwa, hali inayoonesha ongezeko kubwa la ushiriki wa wanawake katika kunufaika na mikopo hiyo.

Serikali imefafanua kuwa mafanikio hayo yamechangiwa na maboresho ya kanuni za utoaji mikopo yaliyowezesha fedha ambazo hazijatumika katika kundi moja kuhamishiwa kwenye kundi jingine lenye mahitaji makubwa ndani ya robo husika ya mwaka wa fedha.

Kutokana na hali hiyo, vikundi vya wanawake vimeendelea kupata mikopo kwa kiwango kikubwa zaidi ikilinganishwa na baadhi ya makundi mengine maalumu.

Waziri huyo alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kufuatilia na kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mpango wa mikopo ya asilimia 10 ili kuhakikisha wanawake wa vijijini wanaendelea kupata fursa za kiuchumi, kuongeza kipato na kuchangia maendeleo ya familia na jamii kwa ujumla.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...