Na Janeth Raphael MichuziTv - Bungeni Dodoma 

Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema kuwa Shilingi ya Tanzania ndiyo fedha halali ya malipo ndani ya nchi, akisisitiza kuwa matumizi yake yanalindwa na Katiba pamoja na sheria za nchi. Amesema Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa taratibu na sheria zinazohusu matumizi ya sarafu ya taifa zinafuatwa ili kuimarisha uchumi wa ndani.

Dkt. Nchemba ametoa kauli hiyo Bungeni jijini Dodoma leo wakati wa kipindi cha Maswali kwa Waziri Mkuu alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalum, Suma Fyandomo. 

Katika majibu yake, Waziri Mkuu alieleza kuwa Shilingi ya Tanzania ndiyo chombo rasmi cha kufanya malipo katika shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazofanyika ndani ya mipaka ya nchi.

Amesisitiza kuwa nafasi ya Shilingi ya Tanzania kama fedha halali ya malipo si suala la hiari, bali ni matakwa ya kisheria yanayopaswa kuheshimiwa na wadau wote wa uchumi, wakiwemo wafanyabiashara, taasisi na wananchi kwa ujumla. Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, matumizi ya sarafu ya taifa yana mchango mkubwa katika kulinda uthabiti wa mfumo wa fedha na kuimarisha uchumi wa nchi.

“Shilingi ya Kitanzania ndiyo malipo halali ndani ya nchi yetu, na hili ni jambo la kikatiba na ni jambo la kisheria,” alisema Dkt. Nchemba wakati akijibu swali hilo mbele ya Bunge.

Kauli hiyo imekuja katika kipindi ambacho kumekuwepo mijadala kuhusu matumizi ya fedha za kigeni katika baadhi ya huduma na shughuli za biashara nchini. Serikali imekuwa ikisisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria na miongozo inayotaka malipo ya ndani kufanyika kwa kutumia sarafu ya Tanzania isipokuwa pale ambapo sheria au kanuni husika zinatoa ruhusa maalumu.

Aidha, msimamo huo wa Serikali unalenga kuendelea kuimarisha hadhi ya Shilingi ya Tanzania, kuongeza imani kwa sarafu ya taifa na kuchochea ukuaji wa uchumi wa ndani. Serikali imeeleza kuwa itaendelea kutoa elimu na kusimamia utekelezaji wa sheria ili kuhakikisha matumizi ya Shilingi ya Tanzania yanaendelea kuwa msingi mkuu wa miamala ya kifedha nchini.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...