Farida Mangube Morogoro
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Dkt. Stella Bitanyi, amewataka wafugaji kuongeza mwitikio wa kuchanja mifugo ili kudhibiti magonjwa, kuongeza uzalishaji na kulinda afya ya binadamu.
Akizungumza Juni 18, 2026 mjini Morogoro katika kikao kati ya TVLA na timu ya Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi (C-SDTP), amesema wafugaji wadogo bado wanaitikia kwa kiwango cha chini kampeni za chanjo licha ya upatikanaji wa chanjo zinazozalishwa na TVLA, huku akisisitiza umuhimu wa elimu kwa wafugaji ili kupunguza magonjwa ya mifugo.
Dkt. Bitanyi amesema mradi wa C-SDTP unapaswa kusaidia utoaji wa elimu kuhusu umuhimu wa chanjo na kushirikiana katika kudhibiti ugonjwa wa tupa mimba (Brucellosis) pamoja na magonjwa mengine yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.
Pia amewahimiza wananchi kutumia maziwa salama kwa kuyachemsha kabla ya matumizi, akibainisha kuwa TVLA inaendelea kuzalisha chanjo, kufanya tafiti za kisayansi, kudhibiti ubora wa viuatilifu vya mifugo na kutoa ushauri wa kitaalamu ili kuongeza afya na tija ya mifugo.
Mratibu wa Kitaifa wa C-SDTP, Lazaro Kapela, amesema mradi huo unatekelezwa katika mikoa minane ya Tanzania Bara na mikoa mitano ya Zanzibar kwa lengo la kutatua changamoto za wafugaji kupitia upatikanaji wa mbegu bora za ng’ombe, malisho bora, huduma za afya ya mifugo na miundombinu ya maji.
Ameongeza kuwa mradi huo pia utawekeza katika vituo vya kukusanyia maziwa ili kuwaunganisha wafugaji na masoko na kuwahakikishia soko la uhakika la bidhaa zao.
Afisa Mwandamizi wa Ufuatiliaji na Tathmini wa mradi huo, Goodluck Masawe, amesema C-SDTP ni mradi wa miaka 10 ulioanza mwaka 2024 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2034 kwa gharama ya dola za Marekani milioni 231.
Amesema mradi huo utanufaisha kaya 140,000 sawa na watu zaidi ya 700,000, ambapo asilimia 40 ni wanawake, asilimia 30 vijana na asilimia tatu ni watu wenye ulemavu watakaofikiwa moja kwa moja na huduma za mradi huo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Benezeth Lutenga Malinda, amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi mikubwa inayolenga kuimarisha mifumo ya afya ya mifugo, maabara na ufuatiliaji wa magonjwa ili kuongeza uzalishaji, ubora na usalama wa maziwa na bidhaa nyingine za mifugo.
Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya wizara, taasisi zake na wadau wa sekta ya mifugo Tanzania Bara na Zanzibar utachangia kuimarisha usalama wa chakula, lishe na kipato cha wafugaji nchini.



.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...