Wakulima nchini wametakiwa kutumia mbegu bora wanapopanda mazao yao ili kuongeza uzalishaji wa mazao yenye ubora wa juu yatakayowezesha kupata bei nzuri kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi.

Wito huo umetolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), CPA. Godfrey Malekano, wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Iringa na Singida yaliyofanyika jijini Dodoma Juni 12, 2026.

CPA. Malekano alisema ubora wa mazao ndiyo msingi mkuu wa upatikanaji wa bei nzuri sokoni, akisisitiza kuwa matumizi ya mbegu bora ni hatua muhimu kwa mkulima kufikia mafanikio ya kiuchumi.

Alisema utaratibu wa wanunuzi kununua mazao moja kwa moja mashambani bila kuyapeleka kwenye mfumo rasmi wa soko umepitwa na wakati, kwani kwa sasa wakulima wana fursa ya kupata bei shindani kupitia mfumo wa TMX uliorasimishwa na Serikali.

“Unapouza mazao nje ya mfumo rasmi, si mkulima pekee anayepoteza fursa ya kupata thamani halisi ya mazao yake, bali hata Serikali inapoteza matokeo ya uwekezaji wake mkubwa katika utoaji wa pembejeo za ruzuku kwa wakulima."

Aliongeza kuwa TMX inaendelea na jitihada za kuhakikisha bidhaa zote za kilimo zinauzwa kupitia soko hilo kama ilivyo katika mataifa mengi yaliyoendelea, Kwa sasa, bidhaa 11 tayari zinauzwa kupitia mfumo huo ikiwemo madini ya Vito.

Aidha, alisema maendeleo ya teknolojia yameongeza uelewa wa wakulima kuhusu mwenendo wa bei za mazao katika soko la dunia kupitia matumizi ya simu janja, hali inayowasaidia kufanya maamuzi sahihi ya biashara.

“Leo hii mkulima anafuatilia bei za mazao akiwa kijijini kupitia simu yake, ndiyo maana wanunuzi wanaotaka kununua kwa bei ya chini hukataliwa kwa sababu wakulima wengi wanatambua thamani halisi ya mazao yao."

Kwa upande wake, Ofisa wa TMX, Justa Martine, alisema kuuza mazao kupitia Soko la Bidhaa Tanzania kuna manufaa makubwa kwa wanunuzi na wauzaji.

Alieleza kuwa mfumo huo hupunguza gharama za mnunuzi kufika eneo la mzigo, huongeza uwazi wa biashara kwa kuonyesha ubora wa bidhaa na mwenendo wa bei sokoni, na pia humpa muuzaji uhuru wa kukubali au kukataa kuuza endapo hajaridhishwa na bei inayotolewa.

TMX inaendelea kuhamasisha wakulima na wadau wa sekta ya kilimo kutumia mfumo wa soko la bidhaa ili kuongeza tija, uwazi na ushindani katika biashara ya mazao nchini.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...