Na: Farida Mangube

Ufugaji wa ng’ombe wa maziwa katika Kata ya Igima, Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe, umeendelea kuwa chanzo kikuu cha mabadiliko ya kiuchumi kwa wananchi, baada ya uzalishaji kuongezeka na ubora wa maziwa kuboreka kutokana na elimu na utafiti unaotolewa na wataalamu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).

Afisa Mifugo wa Kata ya Igima, SHAZI MOSES OKALA, amesema kata hiyo ina zaidi ya wafugaji 300 wa ng’ombe wa maziwa wenye zaidi ya ng’ombe 700, ambapo kwa sasa huzalisha zaidi ya lita 2,500 za maziwa kwa siku. Amesema maziwa hayo hukusanywa kupitia vituo vya ukusanyaji kabla ya kupelekwa kwenye kituo cha kupoozea na baadaye kusafirishwa kwa ajili ya usindikaji.

Yokara amesema kabla ya kuanza kwa elimu na utafiti wa wataalamu wa SUA kupitia Mradi wa NANOCOM, wafugaji walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya magonjwa ya mifugo hususan homa ya kiwele (mastitis), hali iliyosababisha maziwa mengi kuchachuka na kupoteza ubora wake. Hata hivyo, ameeleza kuwa hali hiyo imepungua kwa kiasi kikubwa baada ya wafugaji kupewa elimu ya usafi wa mabanda na mbinu bora za ufugaji.

Ameongeza kuwa elimu hiyo imechangia si tu kuboresha afya ya mifugo, bali pia kuongeza uzalishaji wa maziwa na kipato cha wafugaji, ambapo sasa maziwa mengi yanakidhi viwango vya soko tofauti na ilivyokuwa awali.

Katika hatua nyingine, mfugaji na kiongozi wa kikundi cha Beach Group, Bi. Liones Richard, ameeleza jinsi ufugaji ulivyobadilisha maisha yake tangu alipoanza mwaka 2007 akiwa na ng’ombe mmoja pekee, ambapo kwa sasa anamiliki ng’ombe wanne wanaozalisha zaidi ya lita 20 za maziwa kwa kila ng’ombe kwa siku.

Bi. Liones amesema mafanikio hayo yametokana na matumizi ya mbinu bora za ufugaji na ushauri wa kitaalamu anaoupata, ambao umemsaidia kuboresha lishe ya mifugo, afya ya ng’ombe na usafi wa mabanda, hivyo kuongeza uzalishaji kwa kiwango kikubwa.

Amehitimisha kwa kusema kuwa mafanikio hayo yamemuwezesha kujenga nyumba bora na kuwapatia watoto wake elimu, huku akiwahamasisha wanawake, vijana na wafugaji wengine kuona ufugaji wa ng'ombe wa maziwa kama fursa muhimu ya kiuchumi inayoweza kubadilisha maisha endapo itafanyika kwa weledi na maarifa sahihi.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...