Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
WAZIRI katika Ofisi ya Rais anayeshughulikia Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, amewataka vijana nchini kuzingatia elimu ya fedha akisema ni nyenzo muhimu ya kuwawezesha kiuchumi na kuwapa uwezo wa kushiriki kikamilifu katika agenda ya maendeleo ya taifa.
Nanauka ametoa wito huo leo Mei 5, 2026 wakati akizindua tawi jipya la Benki ya Ushirika (Coop Bank) jijini Dar es Salaam, ambalo ni tawi la sita la benki hiyo tangu kuanzishwa kwake.
Uzinduzi huo umeambatana na kusainiwa kwa makubaliano ya ushirikiano kati ya Coop Bank na Wizara ya Maendeleo ya Vijana yenye lengo la kuwajengea vijana maarifa ya kifedha na kuongeza ushiriki wao katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Nanauka amesema Coop Bank ni daraja muhimu linalowaunganisha vijana na fursa za kiuchumi pamoja na miradi ya maendeleo.
"Elimu ya fedha ni muhimu kwa vijana ikiwa wanataka kuwa huru kiuchumi na kuchangia kwa maana katika maendeleo ya taifa," amesema.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
Aidha, aliwahimiza vijana kujiunga na mifumo rasmi ya kiuchumi na taasisi mbalimbali, akieleza kuwa hatua hiyo itawasaidia kukidhi vigezo vya kupata huduma za kifedha ikiwemo mikopo.
Mtendaji Mkuu wa Coop Bank, Godfrey Ng’urah, amesema tawi la Dar es Salaam ni la nne kufunguliwa mwaka huu. Alibainisha kuwa benki hiyo ilianza shughuli zake ikiwa na matawi matatu katika mikoa ya Mtwara, Kilimanjaro na Dodoma.
Ng’urah amesema benki hiyo inapanga kufungua jumla ya matawi 12 kabla ya mwisho wa mwaka kama sehemu ya mkakati wake wa kusogeza huduma katika vituo vikuu vya biashara nchini.
"Dhamira yetu ni kutoa suluhisho za kifedha kwa Watanzania kwa wakati na kwa kusogeza huduma za benki karibu zaidi na wananchi," amesema.
Ameongeza kuwa kupitia mfumo wa ushirika, benki hiyo inaamini kuwa ifikapo mwaka 2030 itakuwa imeongeza kwa kiasi kikubwa idadi ya wateja wake huku ikitumia teknolojia kuhamasisha maendeleo ya vijana na ujumuishaji wa kifedha.
Pia amesema Coop Bank iko tayari kushirikiana na taasisi za serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo katika juhudi za kuharakisha maendeleo ya taifa.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Coop Bank, Dkt.Joseph Witts, amesema benki hiyo imejizatiti kuunda fursa zitakazowasaidia vijana kuboresha hali zao za kiuchumi.
"Dar es Salaam inachangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa taifa na ina fursa nyingi za uwekezaji na biashara," alisema.
"Kufunguliwa kwa tawi katika jiji hili kutafanya huduma za kifedha zipatikane kwa urahisi zaidi kwa wawekezaji, wafanyabiashara na wateja wetu wanaoongezeka."
Dkt. Witts alisema lengo kuu la benki hiyo ni kuweka maslahi ya wanachama wake mbele huku ikihakikqisha ukuaji endelevu na upanuzi wa shughuli zake.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Abulmajid Nsekela, ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa CRDB Bank, amesema kuendelea kwa upanuzi wa Coop Bank ni mafanikio makubwa kwa harakati za ushirika nchini Tanzania.
"Ufunguzi wa tawi hili la Dar es Salaam ni hatua chanya na ni fursa ya kuhudumia vyama vingi vya ushirika vinavyofanya kazi katika jiji hili," alisema.
Pia amesisitiza umuhimu wa utawala bora, usimamizi madhubuti na matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma bora za kifedha kwa Watanzania.
Kwa sasa, Coop Bank inaendesha matawi sita yaliyopo Dar es Salaam, Dodoma, Moshi, Tabora na matawi mawili mkoani Mtwara.







.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...